China, Marekani waongoza kwa mauzo ya silaha duniani

Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani (SIPRI) yenye makao yake mjini Stockholm,Sweden imeonyesha kuwa makampuni ya silaha ya China na Marekani yalidhibiti soko la silaha duniani kwa mwaka 2019 huku yaking'ara zaidi kati ya makampuni 25 bora duniani, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Picha na Washingtontimes.
Aidha kwa pamoja, mauzo ya silaha na huduma za kijeshi za makampuni hayo 25 zilifanya kiasi cha dola bilioni 361 kwa mwaka 2019, ambacho ni ongezeko la asilimia 8.5 tofauti na mwaka 2018.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya SIPRI makampuni hayo yalifanya hivyo ingawa kwa mara ya kwanza mataifa ya Mashariki ya Kati yameingia kwenye orodha ya wazalishaji wakubwa zaidi 25 wa silaha duniani kwa sasa.

Ripoti hiyo imetaja kuwa,makampuni ya silaha yaliyojikita nchini Marekani yalichukua nafasi tano za mwanzo mwaka 2019, wakati kampuni ya Lockheed Martin, Boeing, Northrop Grumman, Raytheon na General Dyanamics yakifanya biashara ya dola bilioni 166 katika mauzo jumla ya mwaka.

Makampuni 12 ya Marekani yamekuwa miongoni mwa makampuni hayo 25 makubwa zaidi yanayozalisha silaha na kufanya asilimia 61 ya mauzo jumla ya silaha zote duniani.

Wakati huo huo,China imeibuka ya pili kwa kufanya asilimia 16 ya mauzo ya silaha mwaka 2019 ambapo makampuni manne kutoka nchini humo yanayozalisha silaha yamejitokeza miongoni mwa makampuni 25 ya juu, wakati matatu yakiwa kati ya 10 ya mwanzo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mauzo ya silaha ya makampuni hayo manne ya China yaliongezeka kwa asilimia 4.8 kwa mwaka 2019 dhidi ya dola 56.7 bilioni za 2018.

Makampuni hayo ni Aviation Industry Corporation of China ikiwa nafasi ya sita katika orodha hiyo, China Electronics Technology Group Corporation ikiwa nafasi ya nane,China North Industries Group Corporation ikiwa nafasi ya tisa na China South Industries Group Corporation ikiwa nafasi ya 24.

Nan Tian ambaye ni mtafiti mwandamizi kutoka SIPRI amesema kuwa,makampuni ya China yananufaika zaidi na programu za maboresho za Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China.

Ripoti ya SIPRI imeongeza kuwa, kuna uwezekano wa kuwepo kwa makampuni mengine yenye uwezo unaojitosheleza kuorodheshwa miongoni mwa makampuni hayo 25 ya juu zaidi duniani ingawa haikuwezekana kuyaingiza kwenye orodha hiyo kutokana na kukosekana takwimu sahihi na za mlinganisho kuhusu uzalishaji huo wa silaha.

Wakati huo huo, Kampuni ya EDGE ya Umoja wa Falme za Kiarabu imeshika nafasi ya 22 na kufanya asilimia 1.3 ya mauzo jumla ya silaha miongoni mwa makampuni hayo 25 duniani.

Pieter Wezeman ambaye ni mtafiti kutoka taasisi hiyo amesema kuwa, kampuni hiyo iliakisi namna ambavyo mahitaji makubwa ya kitaifa ya bidhaa za kijeshi, lakini pia nia ya kuachana na utegemezi wa mataifa ya Magharibi, yalivyochochea ukuaji wa makampuni ya silaha katika eneo la Mashariki ya Kati.

Nayo Kampuni ya Ufaransa ya Dassault Aviation Group kwa mara ya kwanza imeingia kwenye orodha hiyo ya makampuni 25 makubwa ya uzalishaji silaha. Kampuni hiyo ilichangia ongezeko kubwa katika mauzo ya silaha ya kila mwaka kwa asilimia 105.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news