DED adaiwa kukaidi agizo la Waziri Mkuu, RC Wangabo akasirika

Serikali kupitia miradi yake ya Afya na Usafi wa Mazingira (SWASH) Pamoja na Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa sh. 1,152,557,008.77 kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa madarasa 18, matundu ya vyoo 178, mabweni mawili kwa shule za msingi na sekondari, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Baadhi ya wananchi na viongozi mbalimbali wakishiriki katika songambele ya ujenzi wa madarasa saba ya Shule ya Sekondari Matai wilayani Kalambo.

Halmashauri hiyo ilipatiwa fedha hizo fedha hizo tangu mwezi Juni mwaka 2020, lakini hadi kufikia mwezi Disemba 2020 ujezi wake haujafikia hata asilimia 50 ya ukamilishaji. 

Kutokana na kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amekemea uzembe unaofanywa na viongozi wa halmashauri hiyo huku akisikitishwa na kitendo cha Mkurugenzi wa Halmshauri hiyo, Msongela Palela kuchukua ruhusa ya kuondoka nje ya mkoa huo huku katika halmashauri yake kukikosekana madarasa saba kwa ajili ya wanafunzi 254 waliokosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza katika halmashauri hiyo. 

Mbali na fedha za miradi hiyo wananchi wa Kata ya Matai kwa kushirikiana na halmshauri wameanza ujenzi wa vyumba vya madarasa manne katika shule ya Sekondari Matai ambavyo vinatakiwa kukamilika kabla ya Februari 28, 2021 kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi waliokosa nafasi katika awamu ya kwanza ya uchaguzi wa wananfunzi hao wilayani humo. 

Akizungumza katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya shule za Msingi za Sekondari katika halmshauri hiyo wakati alipokuwa katika Shule ya Sekondari Matai inayotekeleza ujenzi wa madarasa saba na mabweni mawili, RC Wangabo amesema kuwa amekosa imani na utendaji kazi wa halmashauri hiyo baada ya kuona miradi inayogharamiwa na serikali kutomalizika kwa wakati huku miradi inayotekelezwa kwa kushirikiana gharama na wananchi kutokuwa na dalili ya kumalizika. 

“Miezi sita, lakini watu wanafanya utekelezaji kwa asilimia 42 sasa mimi inanipa mashaka,huku tu ambako kuna fedha ujenzi haujakamilika kwa miezi sita, je huku ambako tunaanza msingi na hakuna fedha ni juhudi za wananchi tutakamilisha baada ya muda gani?.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Carolius Misungwi baadhi ya mifuko 30 ya saruji ikiwa ni ahadi ya mkuu wa mkoa katika kuunga mkono juhudi za wananchi katika kukamilisha madarasa ya shule za sekondari wilayani humo. 

"Ninayasema haya kwa uchungu mkubwa kwa sababu angalau mngenitia imani kwamba ile fedha ya Serikali iliyopokelewa shilingi milioni 756 zilikwishakamilika na miundombinu yote inaonekana na iko vizuri kwa ubora wake,lakini hakuna tuko asilimia 42 hatujamaliza na tuna mzigo mkubwa wa haya madarasa tuko kwenye msingi, imani kwangu itatoka wapi kwamba huu ujenzi tutaukamilisha ndani ya miezi miwili, ndugu wanachi tutafika?,”Alihoji Mkuu huyo. 

Aidha, ameutaka uongozi wa halmashauri hiyo kufanya kazi ya ziada ili kutekeleza maagizo ya serikali ili kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanaendelea na masomo yao kama ilivyoelekezwa. 

“Niwaagize uongozi wa Wilaya hususani Mkurugenzi ambaye najua hapa hayupo, watu wameambiwa wasisafirisafiri yeye anasafiri safiri, watu wasiende likizo yeye hayupo hapa, miundombinu haipo, sasa tutafika namna hii, nitakuja tena baada ya wiki mbili kuona hatua ambayo tumeifikia,”amesema. 

Wakati akitoa taarifa ya wilaya hiyo Mkuu wa wilaya hiyo, Carolius Misungwi ameeleza mikakati mbalimbali iliyowekwa na wilaya ili kufanikisha azma ya serikali katika kuhakikisha wanamaliza ujenzi wa madarasa hayo na wanafunzi hao kuendelea na masomo ifikapo Februari 2021. 

“Wilaya imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari za Kalambo, Matai, Msanzi, Mwazye na Mambwe. Vyumba sita vya madarasa vya Shule ya Sekondari Wasichana matai vitatumika kwa muda wakati ujenzi wa vyumba saba unakamilika katika Shule ya Sekondari Matai,”amesema. 

Serikali kupitia miradi yake hiyo imetoa Shilingi 756,278,504.77 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa 18 wilayani Kalambo ambapo vyumba 15 ni vya shule ya Msingi na vyumba 3 vya Shule ya Sekondari Matai ambavyo havijakamilika.

Pia kuna kiasi cha Shilingi 229,678,504 kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo 178 katika shule za msingi na shilingi 6,600,000 kwa ajili ya ujenzi wa matundu sita ya vyoo katika Shule za sekondari na kiasi cha Shilingi 160 kwa ajili ya ujenzi wa Mabweni mawili katika Shule ya Sekondari Matai ambayo nayo hayajakamilika na hivyo kufanya miundombinu yote kuwa katika asilimia 42 ya utekelezaji wake.

Hayo yanajiri ikwa hivi karibuni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alitoa agizo kwa watendaji wote kutokwenda likizo ili kuhakikisha wanasimamia ukamilishwaji wa ujenzi wa madarasa. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news