George Lwandamina ndiye kocha mpya Azam FC

Siku chache baada ya Timu ya Azam FC kumfuta kazi kocha wake, Aristica Cioaba katika msimu wa 2020/2021 kutokana na matokeo mabaya katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, hatimaye wameingia kandarasi na Kocha George Lwandamina, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kocha George Lwandamina. (Picha Africanfootball).

Rai huyo wa Zambia ambaye alikuwa kocha wa Yanga ametua nchini Desemba 2, 2020 kwa ajili ya kuinoa Azam FC ambapo anachukua nafasi ya Cioaba ambaye kwa sasa hayupo katika ardhi ya Tanzania.

Cioaba ambaye alikuwa ndani ya Azam FC kuanzia mwanzo wa msimu alifutwa kazi Novemba 26 Siku moja baada ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga Uwanja wa Azam Complex.

Awali,uongozi wa Azam FC kupitia kwa Ofisa Habari, Zakaria Thabit ulieleza kuwa, mchakato wa kumuondoa Cioaba umefanyika kuanzia timu ilipopoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar na mechi zilizofuata timu ilicheza chini ya kiwango.

"Timu imekuwa ikicheza chini ya kiwango baada ya kupoteza mbele ya Mtibwa Sugar, hata tuliposhinda mbele ya Dodoma Jiji bado hakukuwa na kiwango bora. Kwenye mchezo wetu wa jana dhidi ya Yanga hali ilikuwa hivyo na tumepoteza hivyo makubaliano ya pande zote mbili tumefika makubaliano na kwa sasa Vivier Bahati atakuwa Kaimu Kocha Mkuu," amesema.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) uliochezwa kwenya uwanja huo goli pekee la Yanga SC lilifungwa na Deus Kaseke dakika ya 48 akimalizia pasi ya mshambuliaji, Yacouba Sogne.

Kwa sasa timu hiyo ipo mkoani Mwanza ambapo Desemba 7, 2020 itakuwa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Gwambina FC, Uwanja wa Gwambina Complex ikiwa chini ya kaimu kocha msaidizi, Vivier Bahati.

Lwandamina baada ya kutua nchini amesema kuwa, amekuja ndani ya Azam FC kufanya kazi hivyo mashabiki wampe ushirikiano ili awaletee matokeo bora.

Kocha huyo amesema,amefurahi kuja tena ndani ya Tanzania kwani alikuwepo akaondoka na sasa amerudi tena na imani yake ni kwamba ushirikiano utawawezesha kuyafikia mafanikio makubwa.

Abdlkarim Amin ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Azam FC amesema, wamefanya mchakato wa kumleta Lwandamina baada ya kuukubali uwezo wake na wanaamini atakwenda sawa na sera ya Azam FC ambayo pia inataka matokeo bora.

Post a Comment

0 Comments