HGWT yatwaa tuzo mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na kutoa hifadhi kwa wanasichana wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni katika Wilaya ya Serengeti na Butiama mkoani Mara, Rhobi Samwelly amesema anashukuru shirika hilo kuwa miongoni mwa vinara 16 waliopokea tuzo kutokana na mchango wao kutambuliwa na kuthaminiwa katika mapambano dhidi ya Ukatili wa Kijinsia ikiwemo ukeketaji,ndoa za utotoni na kupigania haki za wanawake na watoto.
Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwely akiwa na cheti mkononi mwake baada ya kukabidhiwa kutokana na mchango wa shirika lake katika kupambana na ukatili wa kijinsia hivyo kuwa miongoni mwa Vinara 16 waliopewa tuzo hiyo. (Picha na DIRA MAKINI).

Shirika hilo, limekuwa miongoni mwa Vinara 16 waliopewa tuzo zilizotolewa na Shirika la Kimataifa la UNFPA Tanzania wakishirikiana na WILDAF na Mkuki kwa kutambua mchango wa mashirika hayo katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ambao bado upo maeneo mbalimbali hapa nchini licha ya Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kukemea vitendo hivyo visivyokubalika kisheria na ni kinyume pia cha haki za binadamu.

Rhobi Samwelly ambaye amepata kutunukiwa tuzo ya heshima ya Malkia wa nguvu kutokana na juhudi zake za kutetea wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni ameyasema hayo wakati akizungumza na DIRAMAKINI leo Desemba 9, 2020.

Amesema, atasimama imara kwa kushirikiana na serikali kupinga vitendo vya ukatili wakati wote ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kwa njia ya mikutano ya hadhara na kwa kuyafikia makundi mbalimbali ya vijana, wanawake na wazee wa kimila ili kwa pamoja kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili.

"Tuzo hii tuliyopewa ni heshima kubwa kwetu Hope for Girls and Women Tanzania mchango wetu unathaminiwa na Mimi Mkurugenzi nimejisikia faraja kubwa sana, juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili zitaendelea, niombe jamii kutoa ushirikiano kuunga mkono mapambano haya kwa dhati ikiwemo kuwafichua wanaofanya ukatili na kuwaripoti katika vyombo vya sheria wachukuliwe hatua, lengo ni kuwa na jamii inayothamini utu, haki na heshima mfano ukeketaji ni kosa kisheria, lakini bado watu wanakeketa lazima sasa wawajibishwe na mwenye kuweza kuwafichua ni mtu yeyote anayeishi katika jamii sio Serikali pekee,"amesema Rhobi. 
Vinara 16 waliopewa tuzo ya kutambuliwa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia wakiwa katika picha ya pamoja akiwemo Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania, Rhobi Samwely. Tuzo hizo zimetolewa na UNFPA Tanzania kwa kushirikiana na WILDAF na Mkuki.

Ameongeza kuwa, kila mwanajamii anawajibu wa kushiriki katika kupambana na ukatili hasa ambao wamekuwa wakifanyiwa watoto wa kike kwa kukeketwa, kuozeshwa katika umri mdogo na watoto wadogo kutumikishwa kinyume cha sheria na kwamba watu wanaofanya vitendo hivyo wasifumbiwe macho kwani huzima ndoto za watoto wa kike kushindwa kuendelea na masomo yao na kujikuta wakiozwa katika umri ambao wanapaswa kuwa shuleni wakipata elimu kwa ajili ya manufaa ya maisha yao na Taifa kwa siku za usoni. 

Shirika la Hope for Girls and Women Tanzanaia kupitia kituo chake cha Nyumba Salama kilichopo Kiabakari wilayani Butiama na Kituo Cha Nyumba ya Matumaini kilichopo Mugumu wilayani Serengeti mkoani Mara vimepokea wasichana wapya wapatao 107 hadi sasa waliokimbia ukeketaji kutoka katika familia zao wakiwemo waliofanya mtihani wa darasa la nne, darasa la saba na kuhitimu elimu ya msingi, mtihani wa kidato cha pili.

Ambapo kipindi cha mwezi Desemba ukeketaji hufanyika kwa kiwango kikubwa kutokana na watoto kuwa likizo hivyo mwanya huo hutumiwa na baadhi ya wazazi na walezi wanaokumbatia mila hiyo.

James Lucas na Justine Omary wakazi wa Musoma wakizungumza kwa nyakati tofauti na DIRAMAKINI wamepongeza mchango wa Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania katika kupambana na ukatili wa kijinsia hususan ukeketaji na ndoa za utotoni kwa kuwasaidia kuwahifadhi mabinti wanapokimbia kutoka makwao. 

Wamesema shirika hilo linatekeleza kwa ufanisi mkubwa matakwa ya Serikali katika kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia na wameomba pia kila mwananchi kushiriki kwa nafasi yake kuunga mkono juhudi za Serikali katika kumaliza vitendo vya ukatili nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news