HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. HUSSEIN ALI MWINYI, RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, KATIKA HAFLA YA KUMUAPISHA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS MHESHIMIWA SEIF SHARIF HAMAD - IKULU ZANZIBAR 08 DISEMBA, 2020

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa hafla ya kumuapisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, hafla hiyo imefanyika leo Desemba 8,2020 katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad;

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla;

Makamu wa Pili wa Rais,

Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid;

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar,

Mheshimiwa Omar Othman Makungu;

Jaji Mkuu wa Zanzibar,

Mheshimiwa Dk. Mwinyi Talib Haji;

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar,

Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara mbali mbali za SMZ,

Dk. Abdulhamid Yahya Mzee;

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi,

Mheshimiwa Idrisa Kitwana Mustafa;

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi,


Mheshimiwa Dk. Abdalla Juma Saadalla Mabodi;

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar,

Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe;

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo,

Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Mliohudhuria,

Ndugu Viongozi wa Dini,

Ndugu Viongozi wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama,

Ndugu Viongozi Wote wa Chama na Serikali,

Ndugu Waandishi wa Habari,

Wageni waalikwa,

Mabibi na Mabwana,

Assalam Aeikum,

Ndugu Viongozi na Wageni Waalikwa,

Awali ya yote, namshkuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Aradhikwa kutujaalia afya njema na kuweza kukutana hapa Ikulu, kwa ajili ya hafla hii muhimu ya kumuapisha Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, ambae juzi nilimteua kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane. Nakushukuru Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad Makamu wa Kwanza wa Rais, kwa kukubali uteuzi wangu. Ridhaa yako imeniwezesha kutimiza matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 katika Ibara ya 39 - (1), nakuuu: Kutakuwa na Makamu Wawili wa Rais ambao watajulikana kama Makamo wa Kwanza wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais.

Hatua hii muhimu imekamilisha uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane ninayoiongoza.

Nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad kwa kupendekezwa na Chama chake cha ACT Wazalendo ili ateuliwe kushika nafasi ya Makamo wa Kwanza wa Rais. Kupendekezwa kwa jina lake, na kuteuliwa kwake ni ushahidi usio na shaka wa imani kubwa ambayo wanachama na viongozi wa ACT wamewekeza juu yake. Nami kwa kuheshimu na kutambua uzito wa imani hiyo kwake, na imani yangu kwake, nikamteua bila kigugumizi chochote, kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Ndugu Viongozi na Wageni Waalikwa,

Tarehe 2 Novemba, 2020 niliapa katika Uwanja wa Amaan, kuwa Rais wa Awamu ya Nane wa Zanzibar. Katika kiapo changu kile, pamoja na mambo mengine, niliapa kuilinda na kuingoza nchi yetu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Katiba yetu, Kifungu cha 9 (3) inaelekeza (nanukuu), “Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa umoja wa kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia”. Aidha, Kifungu 39 (3) kinanitaka, kumteua Makamo wa Kwanza wa Rais kutoka Chama kilichopata nafasi ya pili katika uchaguzi, na chenye idadi ya kura zaidi ya asilimia 10.

Hapana shaka kuwa uteuzi huu nilioufanya umezingatia na kutimiza matakwa ya Katiba yetu. Mbali na kuwa ni takwa la Katiba, binafsi, mimi ni muumini wa umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu na maridhiano. Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa maridhiano ni njia nzuri ya kujenga umoja wa kijamii na ustawi wa nchi na wananchi wake. Ni jambo linalowaleta watu pamoja, linaloileta nchi pamoja, linalotuhakikishia amani na mshikamano wa kudumu.

Kutokana na ukweli huo, nilielezea katika hotuba yangu ya kufunga Kampeni zangu pale Kibandamaiti na pia katika siku ya Kufungua Baraza la Wawakilishi juu ya dhamira yangu na utayari wangu wa kuyaendeleza maridhiano na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Nilitumia fursa hizo pia kufafanua matumaini yangu kuwa, kizazi cha leo cha Wazanzibari ambao asilimia 93 wamezaliwa baada ya Mapinduzi na Muungano, kinayo dhima ya kipekee ya kufunga ukurasa wa uhasama na chuki, na kufungua ukurasa mpya wa upendo na maridhiano. Matamanio yangu, bila shaka na ya wengi wanayoitakia mema Zanzibar yetu, ni kuondoshwa kwa majeraha na madonda ya historia yetu ya Zanzibar, ambayo yameendelea kuwa mtihani kwetu mara kwa mara katika chaguzi zetu.

Ndugu Viongozi na Wageni Waalikwa,

Katika kuyaendeleza na kuyastawisha maridhiano, uko wajibu wa viongozi, uko wajibu wa vyama vya siasa na uko wajibu wa wananchi na jamii kwa ujumla. Mimi, naahidi, nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu kuyajenga na kuyadumisha maridhiano kwa maslahi mapana ya nchi yetu. Yale yaliyo ndani ya mamlaka na uwezo wangu, nitayatekeleza bila kigugumizi wala ajizi.

Kwa kuanzia, nimetekeleza maelekezo ya Katiba kwa kuwafikia wenzetu wa ACT na kuwakaribisha kuunda Serikali. Aidha, kwa mamlaka niliyonayo kwenye Kifungu cha 66 cha Katiba ya Zanzibar, nimewateua jana tarehe 7 Desemba, 2020, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui na Mheshimiwa Omar Said Shaaban kuwa Wawakilishi kutoka miongoni mwa nafasi 10 nilizopewa za kuteua Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Aidha, nitashauriana na Mheshimiwa Makamo wa Kwanza wa Rais juu ya kujaza nafasi zilizobaki katika Baraza la Mawaziri na namna bora ya kuendesha Serikali yetu ya Umoja wa Kitaifa.

Ndugu Viongozi na Wageni Waalikwa,

Maridhiano ya kweli yanajengwa kwa mambo makuu matatu: Kwanza ni dhamira. Pande zote mbili zilizotofautiana ni lazima kuwa na udhati katika kufanikisha na kuendeleza maelewano baina yao. Maridhiano ya ukweli hayawezi kupatikana na kuwa endelevu iwapo wahusika na wadau wote hawana dhamira ya kweli ya kufikia, kufanikisha na kuendeleza maridhiano hayo.

Pili, kuvumiliana, kustahamiliana na kusahau yaliyopita. Waswahili walisema, “Yaliyopita si ndwele tugange yajayo”. Maridhiano yoyote ya kijamii hayawezi kudumu iwapo kila siku tutakuwa tunakumbushana kwa mambo ambayo yamepita. Ujasiri wa maridhiano ni kusahau yaliyopita na kutotonesha vidonda kwani vidonda vikitoneshwa kila mara haviwezi kupona.

Na tatu, kujenga utamaduni wa kuaminiana. Maridhiano yoyote hayawezi kudumu iwapo pande mbili zitakuwa haziaminiani na kila wakati kutafuta sababu ya kutupiana lawama na kutoana kasoro.


Ndugu Viongozi na Wageni Waalikwa,

Nafahamu kwamba uamuzi wa Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, umezingatia ushauri na maoni kutoka kwa viongozi na wananchama wa chama Chake. Maamuzi haya yamefanyika kwa kufuata taratibu za Chama cha ACT – Wazalendo na baada ya kufanyika vikao mbali mbali. Kwa hivyo nachukua fursa hii, kutoa shukurani kwa viongozi na wafuasi wa Chama hicho kwa mchango wao katika kufikia kufanyika maridhiano na wakaweza kushirikiana na Chama cha Mapinduzi katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Awamu ya Nane.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,

Kwa upande wangu, maamuzi haya yamefikiwa kwa kuzingatia mawazo, maeleke na busara kutoka viongozi wa Chama Changu, CCM na siyo maamuzi ya peke yangu. Natoa shukurani kwa viongozi wenzangu wa CCM kwa mawazo yao na maelekezo yao hadi tukaweza kufikia katika hatua hii tunayoishudia hivi sasa. Mafanikio hayo ni kielelezo cha ukomavu wa CCM katika kuendesha siasa bora hapa nchini.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi,

Sisi viongozi kila wakati hatuna budi kuzingatia na tufahamu kwamba maslahi ya wananchi ndio jambo la msingi. Tafauti zetu, kama ndogo au kubwa, zisiwe kikwazo cha maendeleo ya wananchi na nchi yetu kwa jumla. Katiba ya Zanzibar imeeleza kwamba ‘Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe’, Bila ya shaka tumeweza kufikia hatua hiyo kwa sababu tunauelewa ukweli huo wa kikatiba. Nasaha zangu kwa wananchi, ni kwamba sote tuwe kitu kimoja na tuunge mkono juhudi hizi zenye lengo la kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa.

Ndugu Viongozi na Ndugu Wananchi

Nimalizie kwa kusema kuwa, pamoja na mimi kuahidi kutekeleza yale yaliyo ndani ya uwezo wangu, mafanikio ya maridhiano yetu yatategemea sana utayari wa vyama vyetu na utayari wa wananchi wetu kuzipa kisogo tofauti zetu na kuyatazama matumaini yaliyo mbele yetu. Mimi na Mheshimiwa Maalim Seif tumeonyesha utayari huo. Ninyi nanyi ridhianeni, kila mmoja kwa nafasi yake. Tuijenge Zanzibar mpya. Zanzibar yenye mshikamano, Zanzibar yenye maelewano na Zanzibar yenye neema tupu. Mimi ninayo matumaini makubwa sana juu ya huko tuendako.

Nakushukuru tena Mheshimiwa Makamu wa Kwanza Rais, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuheshimu na kutimiza matakwa ya Katiba na kwa moyo wako wa maridhiano. Nakishukuru Chama chako kwa ushirikiano ambao kimekupa. Nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi na kwa namna ya kipekee, Mwenyekiti wangu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa baraka zao na kuunga mkono hatua hii. Bila kuwasahau, wananchi wa Zanzibar kwa kuungana nasi katika hatua nyingine muhimu ya kuijenga Zanzibar Mpya.

Mungu Ibariki, Zanzibar,

Mungu Ibariki, Tanzania.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza!

Post a Comment

0 Comments