IGP Sirro afanya mabadiliko makamanda wa polisi

Simon Sirro ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania leo amefanya mabadiliko ya makamanda wa mikoa ya kipolisi ya Lindi, Morogoro, Tabora na Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Wakati huo huo, IGP Sirro amewahamisha vituo vya kazi maofisa waandamizi wa jeshi hilo nchini.

Msemaji wa jeshi hilo, David Misime amethibitisha hayo leo Desemba 3,2020 kupitia taarifa aliyoitoa kwa umma.

Ameeleza kuwa, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Edward Bukombe amepelekwa makao makuu ya Polisi Kitengo cha Picha na Video.

Aidha, nafasi yake imechukuliwa na Ramadhan Kingai aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha.

Wakati huo huo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Wilbroad Mutafungwa ambaye alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro amekuwa Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini na nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Fortunatus Muslim.

Pia aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, Stanley Kulyamo amepelekwa Shule ya Lolisi Moshi mkoani Kilimanjaro kuwa Afisa Mnadhimu wa chuo hicho na nafasi yake ikichukuliwa na Mtatiro Kitinkwi ambaye awali alikuwa Afisa Mnadhimu shuleni hapo.

Pia Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa amerudishwa makao makuu ya Polisi Dodoma kuwa afisa mnadhimu katika Kamisheni ya Ushirikishwaji wa Jamii na nafasi yake imechukuliwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Safia Shomari ambaye alikuwa Afisa Mnadhimu namba moja Mkoa wa Mwanza.

Hata hivyo, katika mabadiliko hayo, IGP Sirro amemhamisha Naibu Kamishna wa Polisi, Mpinga Gyumi kutoka Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini makao makuu ya polisi Zanzibar na kuwa mkuu wa utawala wa rasilimali watu huku aliyekuwa mkuu wa utawala na rasilimali watu, Faustine Shilogile akipelekwa kuwa naibu mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai makao makuu ya polisi Dodoma.

Kamanda Shilogile amechukua nafasi ya naibu kamishna wa polisi, Charles Kenyella ambaye amestaafu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Naibu kamishna wa polisi, Lucas Mkondya amehamishwa kutoka idara ya maendeleo ya milki makao makuu ya polisi kuwa kaimu kamishna wa fedha na lojistiki na nafasi yake kuchukuliwa na naibu kamisha wa jeshi hilo, John Gudaba.

Post a Comment

0 Comments