Keeway Motor yaidhamini Nyota FC ya Arusha

Kampuni inayojishughulisha na utengenezaji wa pikipiki na vifaa vyake ya Keeway Motor imeingia mkataba wa kudhamini timu ya mpira wa miguu ya Nyota FC ya jijini Arusha, anaripoti Mwandishi Diramakini (Arusha).

Msimamizi wa tawi la Kampuni Keeway Motor inayotengeneza pikipiki na vifaa vyake Mkoa wa Arusha, Lydia Kaguru (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wakisaini mkataba waudhamini kwa timu ya Nyota FC. Kulia ni Kaimu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha, Emanuel Antoni na kushoto ni Meneja wa timu hiyo, Thobias Julius.

Msimamizi mkuu wa tawi la kampuni ya Keeway mkoani Arusha,Lydia Kaguru amesema kuwa, wameamua kuidhamini timu hiyo ikiwa ni njia moja wapo ya kuinua vipaji vya vijana nchini.

Kaguru amesema kuwa,wameingia mkataba wa mwaka mmoja kudhamini timu hiyo na kila mwaka wanatarajia kutumia shilingi milioni 10 na mkataba huo unaanza kufanya kazi Januari Mosi, 2021ingawa tayari wameanza kuwapatia vifaa zikiwemo jezi.

Amesema, kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kila inapotoa huduma imekuwa ikidhamini michezo na hata kuwezesha huduma za kijamii kwani kwa sasa wanazihudumia nchi zaidi ya 80 duniani kupitia pikipiki zao na vifaa vyake.

Pia amesema mbali na udhamini, wachezaji na mashabiki watapata nafasi za kujaribu na kutumia pikipiki zao bila malipo yoyote endapo watakuwa na uhitaji wowote wa usafiri.

Naye Meneja wa Nyota FC, Thobias Julius ameishukuru kampuni hiyo kwa udhamini huo na kubainisha kuwa timu hiyo awali ilikuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kukosa nauli za wachezaji za kwenda kwenye mechi,jezi pamoja na vifaa vingine.

Naye Kaimu Katibu Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Arusha, Emanuel Antoni amesema kuwa wamepata faraja kuona kunawadhamini wanajitokeza kudhamini timu za ligi za chini pamoja na zile za mchangani huku akitoa wito kwa makampuni mengine kujitokeza kufanya hivyo.

No comments

Powered by Blogger.