Kenya, Somalia zalipizana visasi kimya kimya

Mvutano wa kidplomasia baina ya Kenya na Somalia umezidi kushika kasi, baada ya Serikali ya Somalia kusimamisha utoaji wa vibali vinavyotolewa kwenye uwanja wa ndege nchini humo kwa wageni kutoka Kenya, anaripoti Mwandishi Diramakini (Mogadishu).

Uamuzi huo umefikiwa Desemba 7, 2020 ambapo Gazeti la Daily Nation limedokeza kuwa amri hiyo itaanza kutekelezwa Desemba 13, mwaka huu, hivyo Somalia imewashauri wote wanaosafiri nchini humo kuomba Visa kwenye ubalozi wake jijini Nairobi.

Licha ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa kumdokeza Mwandishi Diramakini kuwa, hatua hiyo ni moja wapo ya fukuto la mzozo wa kidplomasia baina ya pande mbili hizo, Ofisi ya Uhamiaji ya hapa nchini Somalia imesema kuwa, hatua hiyo imechukuliwa kutokana na tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Duru za habari zinabainisha kuwa,watu wenye vyeti vya kusafiria vya kidiplomasia watahitajika kupata idhini kutoka kwa Wizara ya Mambo ya Nje hapa mjini Mogadishu kabla ya kusafiri kuingia nchini hapa.

Novemba, mwaka huu Serikali ya Somalia ilifungua tena ubalozi wake mjini Nairobi baada ya kufungwa kwa miaka 10 kufuatia ushindi wa kesi dhidi ya mwekezaji binafsi aliyekuwa amenunua jengo la ubalozi kwa njia ya magendo wakati mapigano yakiendelea Somalia.

Jengo la ubalozi hilo lililopo eneo la Westlands mjini Nairobi, lilinunuliwa mwaka 1972 na limekuwa likikarabatiwa kwa miaka miwili iliyopita sasa.

Pia mwaka jana, mgogoro kuhusu umiliki wa eneo la mpaka wa Bahari ya Hindi kati ya Kenya na Somalia uliongezeka baada ya Nairobi kuamua kukata uhusiano wa kidiplomasia na Mogadishu kufuatia madai kwamba Somalia imenadi maeneo ya mafuta yaliopo mpakani.

Nairobi ilitangaza kuwa, inamrudisha nyumbani balozi wake aliyepo Mogadishu, Luteni Jenerali mstaafu Lucas Tumbo ikidai kuwa uamuzi wa Somalia kupiga mnada eneo moja la mafuta mjini London ni sawa na uchokozi dhidi yake na mali yake asili.

Pia Nairobi ilimrudisha nyumbani Balozi wa Somalia nchini Kenya, Mohamed Nur na kuchochea zaidi kesi ilyokuwa inaendelea mjini The Hague, Uholanzi kuwa mgogoro wa kisiasa kati ya Somalia na Kenya.

Aidha, katikati ya mgogoro huo ni eneo lililopo ndani ya bahari Hindi lenye ukubwa wa mraba maili 62,000 ingawa haijulikani ni taifa gani linalomiliki eneo hilo lenye utajiri wa mafuta na gesi asilia.

Serikali ya Kenya ilisisitiza kwamba mpaka huo unakwenda sambamba na mstari wa Latitude na tayari ilikuwa imeuza leseni za uchimbaji mafuta kwa makampuni ya uchimbaji madini katika eneo hilo kabla ya mzozo huo kufukuta.

Mstari wa mpaka wa Somalia unaonyesha eneo lenye pembe tatu la baharini ambalo linamilikiwa na Kenya na ambapo visima hivyo vitatu vipo.

Nakala za mahakamani zilizowasilishwa zinaonyesha kuwa visima hivyo vitatu vilivyopo katika eneo hilo la pembe tatu vilipewa kampuni moja ya Kitaliano na serikali ya Kenya.

Post a Comment

0 Comments