Kocha ataja sababu ya Singida United kushushwa daraja

Edwin Agayi ambaye ni kocha wa Singida United amesema hali mbaya ya kiuchumi ndio sababu iliyopelekea timu hiyo kushushwa daraja,anaripoti  Mwandishi Diramakini.

Ameyasema hayo baada ya timu hiyo kushushwa madaraja mawili baada ya kushindwa kufika uwanjani, kwenye mchezo wa ligi daraja la kwanza dhidi ya Alliance FC. 
Desemba 22, 2020 Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) ilifanya maamuzi ya kuishusha madaraja mawili klabu ya Singida United.

Pia matokeo yake ya michezo yote ilifutwa kwa kosa la kushindwa kutokea uwanjani katika mchezo wa ligi daraja la kwanza dhidi ya Alliance FC. 

Agayi amesema sababu kubwa hasa iliyosababisha timu hiyo kufikia katika hali hiyo ni kutokana na timu kuwa na hali mbaya ya kiuchumi. 

“Kwa kweli changamoto kubwa ilikuwa ni hali ya kiuchumi haya mengine yote yametokea, lakini tatizo kubwa ni hali ya kiuchumi, ambalo lilisababisha kuna wakati timu ilishindwa kusafiri, kuna wakati wachezaji wakawa wanagoma kwenda kucheza kwa sababu kuna kitu walikuwa wanadai hivyo sababu kubwa ilikuwa ni hiyo,”amesema Agayi. 

Alipoulizwa kuhusu nafasi ya viongozi na ukaribu wao na timu amesema kuwa timu ilikuwa haipati huduma nzuri kama hapo awali na yeye alikuwa hajui ni kwa nini, akasisitiza kuwa ilikuwa ni ngumu hata kwa watu wa pembeni kuisaidia timu kwa sababu Singida United ni kampuni hivyo mtu kutoka nje ingekuwa vigumu kuisaidia timu. 

Post a Comment

0 Comments