Ligi Kuu Tanzania Bara yazidi kukolea

Gwambina FC imegawana alama mojamoja na Azam FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Gwambina Complex jijini Mwanza, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Katika mtanange huo wa Desemba 7, 2020 nahodha wa kikosi cha Gwambina FC, Jacob Masawe amesema kuwa haukuwa mpango wao kupata sare kwenye mchezo kwa kuwa walijipanga vema kupata ushindi wachukue alama tatu zote.

Gwambina walionekana kuwa bora kipindi cha pili ambapo walishambulia lango la Azam FC lililowekwa salama na kipa namba mbili Benedict Haule.

Masawe alikosa nafasi mbili za wazi katika harakati za kusaka ushindi kwa timu yake jambo ambalo lilimfanya ashike kichwa mara kwa mara.

Azam FC, nyota wao Ayoub Lyanga amesema kuwa ni matokeo kama yalivyo matokeo mengine ndani ya uwanja na hawakuwa na chaguo kwa kuwa walipambana kwa nguvu zote.

Wanalambalamba hao pia walikosa nafasi za kufunga katika kipindi cha pili na kuwafanya wafikishe alama 27 wakiwa nafasi ya pili baada ya kucheza jumla ya mechi 14.

Gwambina FC wao wanafikisha jumla ya alama 17 wakiwa nafasi ya 10 baada ya kucheza mechi 10 ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Desemba 6, 2020 Wanajangwani Yanga SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuilaza Ruvu Shooting mabao 2-1 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Manispaa ya Temeke,Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mrundi, Cedric Kaze akisaidiwa na mzawa, Juma Mwambusi inafikisha alama 34 katika mchezo wa 14 na kuendelea kuongoza Ligi KuuTanzania Bara kwa alama saba zaidi ya Azam FC wanaofuatia, ambao wamecheza mechi 14.

Ruvu Shooting wanabaki nafasi ya nne na alama zao 23 za mechi 14, wakizidiwa wastani wa mabao tu na mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wamecheza mechi 11 hadi sasa.

Michael Sarpong ndiye alikuwa nyota wa mchezo huo ambapo alifunga bao la kwanza kipindi cha kwanza na kusababisha la pili kipindi cha pili.

Nyota huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 31 kwa shuti la mguu wa kulia kutoka umbali wa karibu mita 10 akimalizia mpira uliookolewa na beki Juma Said Nyosso kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na winga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tuisila Kisinda kutoka upande wa kulia.

Refa Ludovic Charles wa Mwanza aliyekuwa anasaidiwa na Geofrey Msakila wa Geita na Robert Luhemeja wa Mara akawapa Yanga penalti dakika ya 57 baada ya beki wa Ruvu Shooting, Renatus Ambroce kuunawa mpira uliopigwa na kiungo Mkongo Tonombe Mukoko, lakini shuti la kiungo Deus Kaseke likaokolewa na kipa Abdallah Rashid.

Mshambuliaji David Richard Ulomi akaisawazishia Ruvu Shooting dakika ya 60 baada ya kuunasa mpira uliopigwa fyongo na beki wa Yanga SC, Bakari Nondo Mwamnyeto aliyekuwa anataka kumpasia Nahodha wake, Mghana Lamine Moro.

Beki Cassian Ponera akajifunga kwa kichwa dakika ya 66 kuipatia Yanga bao la pili aliporuka na Sarpong kuzuia krosi ya chini chini ya winga wa zamani wa AS Vita ya kwao, Kinshasa, Kisinda.

Metacha Mnata, Kibwana Shomary, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarpong/Ditram Nchimbi dk85, Deus Kaseke/Haruna Niyonzima dk71 na Yacouba Sogne ndiyo walikuwa wameunda kikosi cha Yanga.

Huku Abdallah Rashid, Hamad Kabasele/William Patrick dk72, Renatus Ambroce/Eradius Salvatory dk87, Cassian Ponera, Juma Nyosso, Zuberi Dabi, Abraham Mussa, Mohammed Issa ‘Banka’/ Moses Shaaban dakika ya 87, Shaaban Msala, Fully Zulu Maganga na David Richard wakiunda kikosi cha Ruvu Shooting.

Wakati huo huo, kabla Riffat Msuya ndani ya dakika saba aliipa ushindi wa 1-0 Mtibwa Sugar dhidi ya Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Kwa ushindi huo, Mtibwa Sugar imefikisha alama 16 baada ya kucheza mechi 14 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 13, wakati Mwadui inabaki na alama zake 10 za mechi 14 katika nafasi ya 17 kwenye ligi ya 18, ambayo mwisho mwa msimu timu nne zitateremka daraja.

Mechi nyingine ya Ligi Kuu hiyo ilikuwa ni Ihefu SC ambayo imelazimishwa sare ya 1-1 na JKT Tanzania Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Joseph Kinyozi alianza kuifungia Ihefu SC dakika ya 46, kabla ya Hassan Twalib kuisawazishia JKT Tanzania dakika ya 90 kabla ya kumalizika kwa mchezo huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news