Tanzania Prisons, Yanga SC zagawana alama, Azam FC yang'ara

Wanajangwani, Yanga SC leo wamegawana alama katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu baada ya kulazimisha sare ya 1-1 na wenyeji, Tanzania Prisons, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Mtanange huo umepigwa katika Uwanja wa Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa huku hali ya hewa ikitajwa kuwa kikwazo.

Yanga SC kwa ushindi wa leo inafikisha alama 44 baada ya kucheza mechi 18 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa alama tisa zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi tatu mkononi.

Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, Tanzania Prisons wakawashitua Yanga SC kwa bao la Jumanne Elfadhili dakika sita tu ndani ya kipindi cha pili akimalizia kazi nzuri ya Nurdin Chona.
Yanga SC walikafanikiwa kujinasua dakika 12 kabla ya filimbi ya mwisho, mkombozi akiwa na mchezaji mpya kutoka Burundi, Said Ntibanzokiza.

Hili linakuwa ni bao la pili kwa Ntibanzokiza ambaye ni ingizo jipya, bao lake la kwanza alifunga mbele ya Dodoma Jiji.

Wakati huo huo, mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Azam FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Polisi Tanzania bao pekee la Ismail Aziz dakika ya 88 Uwanja wa Chuo cha Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Pamoja na ushindi huo, Azam FC inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga SC,Mzambia George Lwandamina inabaki nafasi ya tatu na pointi zake 32 baada ya mechi 17.

Aidha, Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga bao la dakika ya 76 la Rashid Chambo limewanusuru wenyeji, Coastal Union kulala mbele ya Namungo FC ya Ruangwa mkaoni Lindi iliyotangulia kwa bao la Iddi Kipagwile dakika ya 10 timu hizo zikitoa sare ya 1-1.

Post a Comment

0 Comments