Yanga SC yaichapa Ruvu Shooting 2-1

 Matangazo ya moja kwa moja baina ya Yanga SC leo Desemba 6, 2020  dhidi ya Ruvu Shooting katika  Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuilaza Ruvu Shooting mabao 2-1 usiku huu Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Yanga SC inayofundishwa na kocha Mrundi, Cedric Kaze akisaidiwa na mzawa, Juma Mwambusi inafikisha pointi 34 katika mchezo wa 14 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi nane zaidi ya Azam FC wanaofuatia, ambao hata hivyo wamecheza mechi 13.

Ruvu Shooting wanabaki nafasi ya nne na pointi zao 23 za mechi 14, wakizidiwa wastani wa mabao tu na mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wamecheza mechi 11 tu.

Nyota wa mchezo wa leo alikuwa ni mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong aliyefunga bao la kwanza kipindi cha kwanza na kusababisha la pili kipindi cha pili.

Sarpong alifunga bao la kwanza dakika ya 31 kwa shuti la mguu wa kulia kutoka umbali wa karibu mita 10 akimalizia mpira uliookolewa na beki Juma Said Nyosso kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na winga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Tuisila Kisinda kutoka upande wa kulia. 

Refa Ludovic Charles wa Mwanza aliyekuwa anasaidiwa na Geofrey Msakila wa Geita na Robert Luhemeja wa Mara akawapa Yanga penalti dakika ya 57 baada ya beki wa Ruvu Shooting, Renatus Ambroce kuunawa mpira uliopigwa na kiungo Mkongo Tonombe Mukoko, lakini shuti la kiungo Deus Kaseke likaokolewa na kipa Abdallah Rashid.

Mshambuliaji David Richard Ulomi akaisawazishia Ruvu Shooting dakika ya 60 baada ya kuunasa mpira uliopigwa fyongo na beki wa Yanga SC, Bakari Nondo Mwamnyeto aliyekuwa anataka kumpasia Nahodha wake, Mghana Lamine Moro. 

Beki Cassian Ponera akajifunga kwa kichwa dakika ya 66 kuipatia Yanga bao la pili aliporuka na Sarpong kuzuia krosi ya chini chini ya winga wa zamani wa AS Vita ya kwao, Kinshasa, Kisinda.

Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Metacha Mnata, Kibwana Shomary, Yassin Mustapha, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Tuisila Kisinda, Feisal Salum, Michael Sarpong/Ditram Nchimbi dk85, Deus Kaseke/Haruna Niyonzima dk71 na Yacouba Sogne.  

Ruvu Shooting; Abdallah Rashid, Hamad Kabasele/William Patrick dk72, Renatus Ambroce/Eradius Salvatory dk87, Cassian Ponera, Juma Nyosso, Zuberi Dabi, Abraham Mussa, Mohammed Issa ‘Banka’/ Moses Shaaban dk87, Shaaban Msala, Fully Zulu Maganga na David Richard.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news