Liverpool yainyoosha Crystal Palace kwa mabao 7-0

Klabu ya Liverpool imeonyesha nia ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya kuichapa Crystal Palace mabao 7-0, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Crystal Palace dhidi ya Liverpool. (Picha na GETTY IMAGES). 

Mtanange huo wa Desemba 19, 2020 umepigwa katika dimba la Selhurst Park jijini London, Uingereza ambapo hii ni mara ya kwanza kwa Liverpool kufunga jumla ya mabao saba tangu 1991.

Pia ushindi huo umetosha kuwasahulisha mashabiki wa Liverpool kichapo cha 7-2 ambacho kikosi chao kilipata kutoka Aston Villa kwenye EPL ugenini mwezi Oktoba, mwaka huu. 

Kupitia kambumbu hilo safi, Liverpool wameonekana kushambulia sana wenyeji wao baada ya kila dakika, hatua ambayo imewawezesha kupata ushindi mnono.

Siku mbili baada ya kutawazwa Kocha Bora wa Mwaka 2020 katika tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kocha Jurgen Klopp alimpa chipukizi Takumi Minamino fursa ya kuanza mechi katika kikosi cha kwanza na kumweka benchi fowadi Mohamed Salah. Ilikuwa mara ya kwanza kwa benchi ya klabu za EPL kuungwa na wachezaji tisa wa akiba. 

Takumi Minamino amewafungulia Liverpool ukurasa wa mabao katika dakika ya tatu. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa nyota huyo kufunga katika EPL baada ya miezi 12. 

Sadio Mane na Roberto Firmino walifunga mabao mengine ya Liverpool katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, Mane alionekana kukerwa na hatua ya kuondolewa kwake uwanjani katika kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Salah katika dakika ya 57. 

Jordan Henderson alipachika nyavuni goli la nne la Liverpool kabla ya Roberto Firmino kupachika wavuni la tano. Mohamed Salah amewaongezea mauumivu zaidi vijana wa Crystal Palace kwa mara nyingine katika dakika za 81 na 84. 

No comments

Powered by Blogger.