Baada ya Desemba 3, 2020 kundi la watalii 37 kutoka nchini Japan kuwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kutalii sambamba na kufanya mikutano ya mafunzo,Wajapan hao wamevutiwa na fursa zilizopo Tanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Watalii hao wanaofahamika kama Klabu ya Mabilionea (Billionaires Club) watakuwepo nchini kuanzia tarehe 3 hadi 10 Dieemba, 2020. Watalii hawa ambao watatembelea vituo mbalimbali vya utalii nchini ni viongozi na wamiliki wa makampuni kutoka katika sekta mbalimbali nchini Japan.
Baadhi ya watalii kutoka nchini Japan wakijanza taarifa kwenye fomu maalumu mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).
Watalii hao mara baada ya kuwasili nchini walipata fursa ya kusikiliza mawasilisho (presentation) kutoka taasisi mbalimbali kama vile Mamlaka ya Hifadhi Tanzania, Kituo cha Uwekezaji Tanzania na Bodi ya Utalii ya Tanzania ambapo, sambamba kufahamishwa zaidi kuhusu Tanzania, vilevile walielezwa kuhusu fursa na taratibu za kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini.
Watalii kutoka nchini Japan wakiwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA).
Watalii hao wengi walionesha kuvutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo nchini na kuridhishwa na namna Serikali ilivyoandaa mazingira rafiki kwa wawekezaji.
Akizungumza baada ya kusikiliza mawasilisho, Bi. Nanako Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya kutengeneza viungo bandia vya binadamu amesema, amevutiwa na fursa zilizopo katika sekta ya afya na namna Serikali ilivyojiandaa kutoa motisha kwa wawekezaji wa eneo hilo hapa nchini.
Watalii
hawa wametembelea hapa nchini kwa juhudi kubwa za utangazaji na
uhamasishaji utalii zinazoendelea kufanywa na Bodi ya Utalii Tanzania
kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan ambao unafanya
juhudi kubwa ya kufungua soko la utalii la Japan kwa vivutio vya utalii
vinavyopatikana hapa nchini hasa baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona.
Vilevile
watalii hao wametaja mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe
Magufuli katika kupambana na mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Corona (COVID-19), amani iliyopo
nchini, ukarimu wa watanzania na uwepo wa vivutio hadhimu vya utalii
nchini ni miongoni mwa sababu nyingi zilizowafanya kuja kutalii
Tanzania.
Watalii kutoka nchini Japan wakiendelea kufutalia mwasilisho (presentation) kutoka kwa Wataalamu wa Taasisi za Serikali zilizolenga kuwaelezea kuhusu fursa na taratibu za kuwekeza nchini Tanzania.
Akizungumza wakati wa mapokezi ya Watali hao
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania, Haji Thomas Mihayo amesema Ilani
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 inazungumzia kukuza utalii wa
mikutano ili kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea hapa nchini Pamoja
na kuongeza mapato kufikia Dola Billioni 9.
"Sisi Bodi ya Utalii
Tanzania Pamoja na Balozi zetu utekelezaji wa ilani umeshaanza mara
moja, kwani katika kipindi hiki cha miaka mitano ya pili ya awamu hii ya
tano ya muheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli tunalengo la kufikia
watalii milioni 5 na utalii wa mikutano ni moja ya aina za utalii
zitakazosaidia kufikia lengo hilo,"amesema Mihayo.