Mama atumia sumu ya panya kuua watoto wake watatu

Jeshi la Polisi mkoani Manyara linamshikilia, Regina Daniel (24 ) mkazi wa Kijiji cha Ruksimanda Kata na Tarafa ya Bashinet wilayani Babati kwa tuhuma za kuua watoto wake watatu kwa sumu ya panya, anaripoti Mwandishi Diramakini (Manyara).

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, ACP Paul Kasabago amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amesema limetokea Novemba 5,2020 majira ya saa tatu za usiku katika Kijiji cha Rukdimanda wilayani humo.

Amesema, mama huyo aliwaua watoto wake watatu kwa kutumia sumu inayodhaniwa kuwa ni ya panya, ambapo alichokifanya alikuwa na ugomvi na mume wake kwa hiyo kwa ajili ya kumkomoa mume wake aliona ni bora akanunue maembe na sumu ya panya ambapo aliipaka kwenye maembe hayo na kuwalisha watoto wake.

ACP Kasabago amewataja watoto hao watatu waliouawa kuwa ni Emmanuel Augustino (7), Emiliana Augustino (4) na Elisha Augustino (1) ambao wote ni watoto wa kuwazaa mwenyewe mama huyo.

Kamanda licha ya kurejea kutoa wito kwa watu kuachana na matukio ya kikatili na mauaji amesema, miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Dareda Mission wilayani Babati, wakisubiria uchunguzi wa daktari na mara baada ya uchunguzi huo kukamilika miili hiyo itakabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko huku hatua zaidi za kisheria zikifuata.

Post a Comment

0 Comments