Mama auawa kwa ugomvi wa machimbo Geita

Watu watatu ambao ni ndugu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita kwa tuhuma za kumuua mama yao wa kambo, Selestina Manyanza (70) kwa kumjeruhi shingoni,ubavuni na mgongoni Novemba 30, mwaka huu majira ya saa mbili usiku,anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi Mwandakizi Henry Mwaibambe akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).
 
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita Kamishna Mwandakizi Msaidizi Henry Mwaibambe amesema waliokamatwa ni ndugu watatu kutoka familia moja .

Kamanda Mwaibambe amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Juma Honola (62), Kayumbu Honola (59) na Kayombo Honola (27) ambao wote ni watoto wa kambo wa marehemu.

Kamanda Mwaibambe amesema kuwa, tukio hilo likitokea katika Kijiji na Kata ya Nyaruyeye Tarafa ya Busanda Wilaya na Mkoa wa Geita usiku kwa kumvizia marehemu na kumjeruhi kwa kitu chenye mcha kali.

Amesema kuwa, marehemu akiviziwa akiwa anatoka ndani ya nyumba yake kwenda nje kuoga na kushambuliwa maeneo mbalimbali ya mwili wake na kusababisha kifo chake.

Mwaibambe amesema kuwa, katika uchunguzi wa polisi ulibaini chuma kinachoitwa "moto" kinachotumika na wachimbaji wadogo kuchimba madini ya dhahabu kilikutwa eneo la tukio.

Chanzo cha mauaji hayo kinatajwa na Kamanda Mwaibambe kuwa ni mgogoro wa eneo la kuchimba madini ambalo ni eneo la ardhi inayomilikiwa na familia hiyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Mwaibambe baba wa familia hiyo alikuwa na wake wengi, kwa hiyo watuhumiwa hao walikuwa na mgogoro na mama yao wa kambo ambaye waliona hawatendei haki katika mgawanyo wa ardhi hiyo yenye madini ya dhahabu.

Kutokana na mgogoro huo,watoto hao walikula njama na kumuua mama huyo kwa kumshambulia na kumjeruhi maeneo mbalimbali ya mwili.

Watuhumiwa wote watatu watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa polisi utakapokamilika.

Post a Comment

0 Comments