Manchester United yaichapa Leeds United 6-2

Yametimia, saa chache baada ya kocha Ole Gunnar Solskjaer (47) kusema ana matumaini kikosi chake cha Manchester United kitaimarika zaidi na kurejea kuwa miongoni mwa watetezi wa mataji katika soka la Ulaya ikiwemo Uingereza, majawabu yameonekana, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kiungo Scott McTominay amefanya yake kwa Man United (Picha na KEVIN QUIGLEY). 

Ni baada ya leo Desemba 20, 2020 katika dimba la Old Trafford klabu hiyo kuiadhibu Leeds United 6-2 ambapo kiungo Scott McTominay ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao mawili chini ya dakika tatu za awali katika mchuano huo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

McTominay amewafungulia Man-United nusu dazeni ya mabao baada ya sekunde 67 pekee kabla ya kufunga goli la pili sekunde chache baadaye kwa kukamilisha krosi ya Anthony Martial kupitia kabumbu safi. 

Aidha, Bruno Fernandes na Victor Lindelof walitikisa pia nyavu za Leeds United katika dakika za 20 na 37 kabla ya Liam Cooper kurejesha bao la kichwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza. 

Wakati huo huo, Daniel James alifungia Man-United bao la nne katika dakika ya 65 kabla ya Fernandes kuongeza goli lake la pili kupitia penalti iliyotokana na tukio la Martial kuchezewa visivyo na Pascal Struijk ndani ya sanduku. 

Mtanange huo wa kusisimua umeendelea kuvuta macho na masikio ya mashabiki ambapo ndani ya dakika 73, Stuart Dallas amewapachikia Leeds United bao la pili. Kutokana na ushindi huo mnono wa Man-United umewapeleka katika nafasi ya tatu kwa ponti 26 sawa na Everton walioichapa Arsenal 2-1 katika dimba la Goodison Park jana Desemba 19, 2020. 

Hata hivyo, Leeds United wamebaki katika nafasi ya 14 kwa pointi 17 huku ikwa katika alama nyekundu ya vikosi ambavyo vitashuka daraja msimu huu.

No comments

Powered by Blogger.