Mbunge Biteko aonyesha njia Sekta ya Elimu Bukombe

Doto Biteko ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita na Waziri wa Madini mstaafu amesema anatamani wanafunzi wa shule za sekondari na kutoka mikoa mingine nchini kusoma katika Wiaya ya Bukombe ikiwa ni moja ya kujenga utaifa kwa kuchanganya wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Mbunge wa Jimbo la Bukombe Doto Biteko akiwa amebeba jiwe akiwa na wananchi wa jimbo hilo wakikusanya mawe ya kujenga jengo la utawala katika shule ya Sekondari ya Igulwa jimboni Bukombe. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).
Bunge wa Jimbo la Bukombe, Doto Biteko (mwenye kofia) akiwa anapakia mawe kwenye gari akishirikiana na wananchi wa jimbo hilo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala katika shule mpya ya Kata ya Igulwa jimboni humo. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amesema hayo leo Desemba 2, 2020 wakati wa kukusanya mawe kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala katika shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Igulwa ambayo inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi mwezi Januari,mwakani.

Shule hiyo ina vyumba vya madarasa vilivyokamilika vitano ambavyo vilijengwa kwa nguvu za wananchi pamoja na Mbunge huyo kuchangia mabati yote,saruji mifuko 300 na fedha za mafundi ujenzi.

Mbunge huyo amesema kuwa, Wilaya ya Bukombe ambayo ndiyo jimbo la uchaguzi haikuwa na shule ya kidato cha tano, lakini baada ya kuomba kibali kutoka serikalini kupandisha hadhi shule mbili za sekondari, serikali imewapatia milioni 500 za kuboresha miundombinu ya shule hizo na muda wowote zinaanza kupokea wanafunzi.

Ameongeza kuwa,anatamani wanafunzi wengine wa kutoka mikoa mingine waje kusoma Bukombe na wanafunzi wa Bukombe wapangiwe kusomea mikoa mingine ili kujenga utaifa kwa kuchangamana na kushirikishana mambo mbalimbali kama mila na desturi zetu.

Pia amesema, baadhi ya wanafunzi wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya kipato hafifu cha familia zao hasa kukosa nauli,hivyo ujenzi wa shule hizo maeneo ya karibu utasaidia hata wanafunzi wanaotoka familia hizo kupata elimu kwa urahisi bila kulazimika kusafiri kwenda mbali au mikoa mingine.

Mbunge Doto Biteko (katikati aliyekaa) akiwa na baadhi ya wananchi wakisubiria gari kwa ajili ya kupakia mawe kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari katika Kata ya Igulwa jimboni Bukombe.

Kata ya Igulwa haina shule ya sekondari tangu mwaka 2015 baada ya kugawanywa na kupatikana kata nyingine mbili mpya ambazo ni Katente na Bulangwa zilizobaki zikiwa na sekondari zote.

Wanafunzi wa kata hiyo ya Igulwa ambao kila mwaka wanaochaguliwa kujiunga na sekondari ni 500, lakini wanalazimika kusafiri zaidi ya kilomita tisa kwenda kata jirani kufuata sekondari.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Igulwa,Joseph Msusa amesema, kata hiyo imekuwa na changamoto ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kwenda shule kwa wanafunzi wa sekondari.

Msusa amesema, changamoto wanazopata wanafunzi hao kutokana na umbali wa kwenda shule ni pamoja na kukatisha masomo,watoto kupata mimba pamoja na kipindi cha masika kushindwa kuvuka mto unaofurika maji.

Kiongozi huyo amesema, kutokana na umbali huo,ameishapokea kesi tatu ofisini kwake zinazohusu wanafunzi kupata mimba,hivyo anaamini ujenzi wa sekondari mpya ambayo itakuwa umbali wa kilomita tatu utasaidia kumaliza matatizo hayo.

Mwanafunzi wa Sekondari ya Katente,Majid Kasunzu amemuomba Mbunge Doto Biteko kuwasaidia kwa kuhakikisha shule hiyo inaanza kwa wakati ili waweze kuitumia na kupunguza changamoto wanazopitia.

Amesema, baadhi ya changamoto ni pamoja na kipindi cha mvua kwa kuwa eneo wanaloishi liko mlimani na kuna msitu,kuna mto unaofurika na wanashindwa kuvuka pia kuna wanyama pori kama fisi ambao ni hatari kwao.

Kufuatia changamoto hiyo serikali kwa kushirikiana na wananchi wa kata hiyo wameanzisha ujenzi wa shule ya sekondari Igulwa kwa kujenga vyumba vitano vya madarasa na jengo la utawala.

Mbunge Biteko amesema, kwa sasa mwitikio wa wananchi wa Bukombe kushiriki katika shughuli za maendeleo ni mkubwa hasa katika kazi za kutumia nguvu zao wenyewe kama kusomba mawe au mchanga.

Amesema, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za maendeleo ili wajenge miundombinu ya shule ili serikali iwaletee mahitaji mengine kama walimu,vitabu na kemikali za maabara.

Mheshimiwa Biteko amekuwa Mbunge wa Jimbo la Bukombe tangu mwaka 2015 na amefanikiwa kuwa Naibu Waziri wa Madini na baadaye Waziri Kamili wa wizara hiyo katika Serikali ya Awamu ya Tano kipindi cha kwanza na sasa amerudi bungeni kwa kuchaguliwa kwa awamu ya pili kwa kipindi cha miaka mitano.

Post a Comment

0 Comments