Mbunge Kanyasu, Mwenyekiti wajipanga kuboresha elimu, afya na maji Geita

Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Constantine Morandi wamesema wamejipanga kumaliza changamoto ya uhaba wa madarasa, zahanati pamoja na maji katika Jimbo na Halmashauri ya Mji wa Geita, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
 
Mbunge Constantine Kanyasu amesema miaka mitano iliyopita mwaka 2015 -2020 Halmashauri ya Mji wa Geita ilijenga shule mpya 16 hivyo katika kipindi cha miaka 5 ijayo kwa 2020-2025 kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo watamaliza upungufu wa vyumba vya madarasa au kufikia asilimia 80.Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini, Constantine Kanyasu akiwa anachimba msingi katika ujenzi wa shule mpya katika Mtaa wa Samina Kata ya Mtakuja Geita Mjini, (Picha na Robert Kalokola/ Diramakini).

Kanyasu anasema hayo wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa shule mpya ya msingi katika Mtaa wa Samina Kata ya Mtakuja Mjini Geita ambayo yeye na mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita, Constantine Morandi wameshirikiana na wananchi wa mtaa huo kuchimba msingi.
Kanyasu anasema kuwa, shule hiyo inajengwa ili kunusuru uhai wa watoto wadogo hasa wa madarasa ya chini kama wa darasa la kwanza kwa kutembea umbali mrefu kufuata shule mtaa wa pili wa Mpomvu.

Amesema kuwa, wanafunzi wanatembea zaidi ya kilomita 4 kutoka mtaa wa Samina kwenda mtaa wa Mpomvu na wanapita katika barabara kuu itakayo Mwanza kuelekea Bukoba jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa wanafunzi hao.

Mbunge Constantine Kanyasu amechangia ujenzi kwa kutoa matofali 2000 kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa matatu kwa kuanzia huku Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Constantine Morandi akichangia mifuko ya saruji 50 .

Kanyasu amesema katika kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu aliahidi kujenga shule katika Mtaa huo na kwamba kwa kuwa amepata Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye anapenda kuona vitu vinafanyika,watashikiana kumaliza tatizo la uhaba wa madarasa, zahanati na kutatua changamoto ya maji.

Shule hiyo inaanza kujengwa vyumba saba vya madarasa na ofisi mbili za walimu ambapo wananchi wameshakusanya tripu 30 za mawe na mchanga tripu 10 kwa ajili ya ujenzi huo.
Constantine Morandi ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita akishiriki kuchimba msingi wa shule mpya katika Mtaa wa Samina Kata ya Mtakuja Mjini Geita. (Picha na Robert Kalokola). 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita Constantine Morandi ambaye pia ni Diwani wa kata hiyo,amesema watasimamia ujenzi huo ukamilike mapema ifikapo mwezi Machi mwaka 2021.

Morandi amesema watoto wa mtaa huo wa Samina walikuwa wanatembea kilomita 4 kufuata shule katika Mtaa jirani wa Mpomvu ambapo wanalazimika kupita katika barabara kuu ya kutoka Mwanza kwenda Bukoba ambayo ni hatari kwa usalama wa watoto hao kugongwa na magari.

Aidha, amesema shule ya msingi ya Mpomvu ina wanafunzi 2674 kwa idadi hiyo shule inahitaji kupunguziwa wanafunzi na kati ya hao wanafunzi 1050 wanaotoka mtaa wa Samina kwenda kufuata shule ya Msingi Mpomvu.
Baadhi ya wananchi wa mtaa wa Samina wakishiriki katika kuchimba msingi katika ujenzi wa shule mpya inayoanza kujengwa kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Geita mjini na diwani wa kata ya Mtakuja ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita Constantine Morandi (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Afisa Mtendaji wa kata hiyo Neema Onesmo amesema fedha zaidi ya milioni 100 zitatumika katika ujenzi wa shule hiyo na kwamba kwasasa wameanza na nguvu za wananchi pamoja fedha za ruzuku kutoka kwa vibarua wanaotoka kwenye mtaa huo na kufanya kazi GGML.

Neema Onesmo amesema kuwa,kata hiyo ina mitaa 7 ,shule za msingi 5, hivyo mtaa wa samina ulikuwa unategemea Mtaa wa Mpomvu na kutokana na umbali wanafunzi wengi hasa watoto wa darasa la kwanza walikuwa wanashindwa kufika shuleni kila siku hivyo kuwepo utoro kutokana na uchovu au kuogopa kuadhibiwa na walimu kwa kuchelewa kila siku.

Afisa Mtendaji wa mtaa wa Samina, Deus Bulalu wakati akisoma risala kwa mbunge wa Jimbo la Geita mjini alisema kuwa Shule hiyo ina eneo lenye ukubwa wa ekari 10.5 na mahitaji ya tofali za kujengea maboma 7 ni tofali 6,480 na mifuko ya saruji 162.

Ameongeza kuwa, wananchi wameisha kusanya mawe tripu 30 ,mchanga tripu 10 na kokoto tripu 2 ambapo mtaa huo una kaya 656 na una idadi ya watu 2804 huku wanawake wakiwa 1376 na wanaume 1428.

Zena Nalichika Mkazi wa mtaa wa Samina anasema kuwa watoto wao wanateseka kwa kutembea umbali mrefu kwenda Mpovu lakini pia Kuna hatari ya kugongwa na magari kwasababu wanakatiza katika barabara kuu itakayo Mwanza kwenda Bukoba.

Irene Rukia ambaye ni mjumbe wa serikali ya mtaa wa Samina anasema kuwa maamuzi ya kujenga shule hiyo yalifikiwa na wananchi ili kuweza kuwasaidia watoto wao kutembea umbali mrefu pamoja na usalama wao kwasababu ya kuepuka ajali katika barabara kuu.

Jimbo la Geita mjini ambalo kwa ujumla ndiyo Halmashauri ya mji wa Geita ina jumla ya kata 13 na kwasasa mbunge wa Jimbo hilo ni Constantine Kanyasu na Mwenyekiti wa Halmashauri ni Constantine Morandi ambao wote kwa pamoja wanaahidi kwa kipindi Cha miaka 5 kushughulikia kero za elimu, afya na maji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news