Mganga Mkuu wa Serikali ataka majibu ya sampuli za COVID-19 kwa wasafiri kutolewa ndani ya saa 24

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Abel Makubi ameuagiza Uongozi wa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kutoa majibu ya sampuli za Ugonjwa wa Covid-19 ndani ya saa 24, badala ya saa 72 kwa hospitali zinazopeleka Sampuli hizo au kwa wananchi wanaojitokeza kupima ugonjwa huo kwa nia ya kutaka kusafiri nje ya nchi, ili kuondokana na malalamiko ambayo yamekuwa yakielekezwa kwa maabara hiyo kuwa kuna ucheleweshaji mkubwa wa majibu ya vipimo hivyo, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mganga Mkuu wa Serikali ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na Uongozi wa Maabara hiyo, Waganga wakuu na wasimamizi wa Maabara kutoka Hospital za Rufaa za Serikali na za Binafsi kutoka mkoa wa Dar es salaam mara baada ya kufanya ziara katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya jamii, kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili maabara hiyo.

Prof. Makubi amesema, pamoja na kuweka mifumo mizuri katika maabara hiyo lakini bado kumekuwepo na malalamiko wanayapokea kutoka kwenye baadhi ya hospitali na hata kwa wasafiri wanaofika katika maabara hiyo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, ucheleweshaji ambao umekuwa kero kwa wananchi hao na kamwe hautaweza kuvumiliwa.
“Tafuteni njia mtakayofanya ila hakikisheni kuanzia sasa majibu yote ya Covid-19 yanatolewa ndani ya saa 24 kwa wale wote watakaofanyiwa vipimo kwa Dar es salam na saa 48 kwa mikoani, na lazima suala hili lisimamiwe na wasimamizi wote wa maabara zinazohusika ili kuhakikisha kero hii inaondolewa,"amesema Prof. Makubi. 

Aidha, mfumo wa kufatilia vipimo na majibu kati ya Maabara kuu na Hospitali lazima uboreshwe na kufanyiwa tathimini kila wakati na kila msimamizi atimize wajibu wake bila kuchelewesha. 

Katika hili Prof.Makubi ameutaka uongozi huo kulisimamia kisawa sawa jambo hili na kuhakikisha unaweka mfumo mzuri ambao utaweza kuzifuatilia sampuli zote za Covid-19 ambazo zitafika katika maabara hiyo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.

Katika hatua nyingine Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi ameshangazwa na kitendo cha kupotea kwa baadhi ya sampuli za Covid-19 ambazo zimekuwa zikifikishwa katika maabara hiyo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo, na kushindwa kuelewa inakuwaje sampuli hizo zinapotea na kulazimika kurudiwa, tena kwenye maabara kuu ya taifa ambayo inategemewa na maabara nyingine.

“Kwa hili la kupotea kwa sampuli kwa kweli haliwezi kuvumilika, naelekeza kwa sasa hivi nisisikie tena kuna sampuli yoyote ambayo imepotea, si vyema katika mfumo wa maabara kupoteza kwa sampuli; iwe mwiko kupotea kwa sampuli yoyote ndani ya Maabata kuu ya taifa na maabara zote nchini,"amesema Prof. Makubi.

Kuhusu changamoto ya kuongeza watumishi katika maabara hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali amesema tayari imeanza kufanyiwa kazi na hivi karibuni Maabara Kuu ya Taifa itaweza kupokea watumishi wapya, ambao wataongeza nguvu katika kufanikisha huduma zinazotolewa na maabara hiyo zinakuwa zenye ufanishi. 

Aidha, Serikali inakamilisha mfumo wa TEHAMA ambao utasaidia kuharakisha majibu katika kuwafikia wasafiri na kuwapelekea majibu na vyeti moja kwa moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news