MWENYEKITI WA HALMASHAURI AOMBA TAKUKURU KUZUIA RUSHWA KULIKO KUPAMBANA

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita, Constantine Morandi ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Geita kuongeza nguvu zaidi katika kuzuia vitendo vya rushwa katika halmashauri hiyo kuliko kupambana, anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita Constantine Morandi akila kiapo mbele ya Hakimu katika ukumbi wa Halmashauri ya mji wa Geita (Gedeco). (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Ametoa ushauri huo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya mji Geita cha kwanza kilichofanyika leo katika ukumbi wa GEDECO kwa ajili ya kuapisha madiwani na kuchagua mwenyekiti wa Halmashauri,Makamu wake pamoja na Kamati mbalimbali.

Mwenyekiti Constantine Morandi amesema, Takukuru isisubiri vitendo vya rushwa vitendeke katika halmashauri hiyo badala yake izue kabla ya kutendeka ili kusaidia wananchi waweze kunufaika fedha za miradi ya maendeleo.
Afisa wa Takukuru Mkoa wa Geita, Zabron Sabaya amewataka madiwani kufanya kazi zao kwa kufuata sheria za nchi na kuwa waadilifu muda wote katika kipindi chao cha miaka mitano ili kuepuka kuangukia katika mikono ya taasisi hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Geita, Joseph Lugayila akila kiapo katika ukumbi wa halmashauri hiyo.(Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Amesema kuwa, taasisi hiyo haitamfumbia macho Diwani yeyote ambaye atajihusisha na vitendo vilivyo kinyume na maadili ya uongozi kama vile kutumia madaraka vibaya pamoja na kula rushwa.

Amewataka Madiwani wakati wa kufanya maamuzi mbalimbali kuhakikisha wanatangaza maslahi yao binafsi na kutofanya hivyo itakuwa ni kuvunja sheria za nchi na wanaweza kufikishwa mahakamani.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Fadhili Juma amewataka Madiwani kufanya kazi zao kwa bidii katika kata zao kwani wao ndiyo wanasimamia miradi yote ya Maendeleo kwenye kata zao .

Amewakumbusha kwenda kuendesha vikao vya maendeleo vya kata (WDC) ambavyo vilikuwa havifanyiki baada ya kuvunjwa kwa mabaraza ya madiwani,ili waweze kupanga mipango ya maendeleo.

Mbunge wa Jimbo la Geita, Constantine Kanyasu amewaomba Madiwani kushirikiana katika shughuli zao na kuahidi kushirikiana nao katika kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025.

Baraza la madiwani la Halmashauri ya mji wa Geita lina jumla ya Madiwani 19 ambao wamechagua Mwenyekiti wao Constantine Morandi kwa kura 19 na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Joseph Lugayila aliyepata kura 19 pia zote za ndio.

Post a Comment

0 Comments