Prof.Manya afunga kikao kazi cha maofisa madini nchini

Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya leo Desemba 18, 2020 amekifunga rasmi kikao kazi cha siku tano cha Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini, anaripoti Tito Mselem (WM), Dodoma.
Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya akizunguza jambo katika kikao kazi cha Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Madini jijini Dodoma.
Akifunga kikao hicho, Prof. Manya amewataka Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini kuwa waadilifu katika utendaji wa majukumu yao.

Prof. Manya, amesema Maofisa Madini wote nchini wanatakiwa kuonesha mfano kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa kufuata taratibu na sheria zilizowekwa na Serikali ikiwemo kuonesha ubunifu kwenye kazi zao za kila siku ili kuongeza ufanisi.
Naibu Waziri wa Madini, Prof. Shukrani Manya katikati akiwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Olel (kushoto) na kulia ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.

Pia, Prof. Manya amempongeza Rais Dkt.John Magufuli kwa kumteua kuwa Naibu Waziri wa Madini kitu ambacho hakuwahi kufikiria katika maisha yake.

“Mheshimiwa Rais anatamani migodi mipya ifunguliwe nchini na pia Mheshimiwa Rais anatamani madini yetu ya makaa ya mawe yaanze kuchimbwa, hivyo tuhakikishe tunayafanikisha maono hayo,” amesema Prof. Manya.
Baadhi ya Maofisa Madini Wakazi walioshiriki kikao kazi cha siku tano kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Madini jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa, ndani ya kipindi cha miaka mitatu, Prof. Manya amepata nafasi ya kuteuliwa katika nafasi tano tofauti ambapo Januari 8, 2017 alichaguliwa kuwa Kamishina wa Madini, Juni 1, 2018 alichaguliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Desemba 11, 2020 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Desemba 11, 2020 alichaguliwa kuwa Naibu Waziri wa Madini.

Katika hatua nyingine, Prof. Manya amewapongeza watumishi wote wa Tume ya Madini kwa ushirikiano mkubwa waliomuonesha katika kipindi chote alipokuwa akiwaongoza.

Pia, Prof. Manya ameahidi kumpa ushirikiano na kumshauri Katibu Mtendaji atakayeteuliwa na Mhe. Rais, kwamba kipaumbele chake kiwe kuelekeza fedha katika maeneo yanayotoa matokea chanya katika ukusanyaji wa maduhuli ya serikali.

Aidha, Prof. Manya amewataka wafanyakazi wote wa Tume ya Madini kusaidiana katika shughuli zao na kama kuna moja atakosea au atakosa ubunifu katika shughuli zao inawapasa kusaidiana, kuelekezana na kufundishana ili kuleta tija katika Sekta ya Madini.

Vile vile, Prof. Manya amewataka Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa yote nchini kufanya maamuzi ya haki kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na Serikali.
Naibu Waziri wa Madini Shukrani Manya akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa Tume ya Madini.

“Hakikisheni mnafanyakazi kwa kuzingatia haki, taratibu na sheria msiwaonee watu wala msimpendelee mtu, fanyeni kazi kwa juhudi na ueledi ili mlete tija katika Sekta ya Madini,”amesisitiza Prof. Manya.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango wa Wizara ya Madini, Augustine Olel, amewataka Maofisa Madini Wakazi wa Mikoa yote Tanzania kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa kumtanguliza Mwenyezi Mungu na kuwa waaminifu katika shughuli zao.

No comments

Powered by Blogger.