Rais Dkt. Mwinyi ataja sababu za kuchukua hatua kali

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa hatua anazozichukua sasa lengo lake ni kuleta nidhamu katika matumizi ya fedha za Serikali, anaripoti Mwandishi Diramakini. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi baada ya Swala ya Ijumaa na Kuufungua Msikiti Masjid Nuru Muhammad Bumbwini Tengeza Wilaya kaskazini "B" Unguja leo ambapo swala hiyo Iliswalishwa na Kadhi wa Wilaya ya Mjini Sheikh Othman Ame Chum.(Picha na Ikulu) 

Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Desemba 25, 2020 mara baada ya kuufungua msikiti mpya wa “Noor Muhammad”, ulioko Bumwini Tengeza Mkoa wa Kaskazini Unguja, hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabih. 

Katika hotuba yake Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa, hamtafuti mtu na hakuna atakayeonewa na atahakikisha anatenda haki na alimuomba Mwenyezi Mungu amsaidie. 

Amesisitiza kwamba, fedha za Serikali lengo lake ni kuwasaidia wananchi wote kwa ajili ya huduma za jamii ambazo ziko nyingi zikiwemo ubovu wa marabara, huduma za afya, ukosefu wa madawati pamoja na huduma nyingine. 

Alhaj Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa, fedha za serikali ni lazima zitumike kwa huduma hizo na si kwa wananchi wachache jambo ambalo halikubaliki. 

Amesisitiza kwamba, ataendelea kuchukua hatua hizo na kuahidi kutomuonea mtu ila yule atakayethibitika hajahusika atarejeshwa Serikalini na yule atakayethibitika basi hatua kali zitachukuliwa ili nidhamu iwepo katika nchi ili na watu wajue kuwa fedha za umma ni za watu wote na si kwa mtu mmoja. 

Sambamba na hayo, Rais Alhaj Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba bila ya nidhamu mafanikio hayatapatikana nchini kama ilivyokusudiwa. 

Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi ametoa shukurani kwa wale wote waliohusika katika ujenzi wa msikiti huo huku akiwapongeza wananchi wa Bumbwini kwa kumualika kwenda kuufungua msikiti huo. 

Alhaj Dkt. Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza wananchi wote wa Zanzibar kwa kuendelea kudumisha amani iliyopo. 

Amesema kwamba, kabla ya uchaguzi vingozi wa dini na siasa walisisitizwa kudumisha amani kazi ambayo imefanywa kwa kiwango kikubwa kwa sababu bila ya amani hakuna kitakachofanyika. 

Amesema kwamba, hakuna maendeleo yoyoye yanayoweza kupatikana kama hakuna amani na kuwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea kuidumisha amani waliyonayo. 

Ameongeza kwamba, katika suala zima la utaratibu wa kidemokrasia uliopo kila baada ya miaka mitano vyama vya siasa vinashindanishwa ili yule ambaye sera zake zinakubalika aweze kuongoza nchi. 

Alisema kwamba kwa bahati mbaya ile tafsiri ya demokrasia ambayo maana yake ni kushidanishwa vyama kwa sera ilibadilishwa ikawa ni ugomvi na uhasama miongoni mwa wananchi wa Zanzibar. 

Hata hivyo, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema kuwa, majukwa ya siasa yalitumika kwa kusema kwamba hakuna haja ya kufarakana na badala yake kuwepo ushindani wa hoja na sera na kwa kuhakikisha kunatokea umoja ndipo yakawepo maridhiano. 

Amesema kwamba, kulianzishwa Serikali ya umoja wa kitaifa ili wananchi wote wa Zanzibar wawe ndugu na waweze kufanya kazi kwa pamoja na kufikisha lengo la kuwaletea wananchi maendeleo na si kugombana wala kuhasimiana. 

Amesema kwamba, wapo watu ambao bado hawajawa tayari kuyakubali maridhiano lakini amesisitiza kuwa ipo haja ya kuwaelisha ili wajue kuwa maridhiano yana umuhimu mkubwa katika kuleta umoja ndani ya jamii. 

Amesema kwamba si sahihi kuona Wazanzibari wenyewe kwa wenyewe wanabaguana kwa siasa, dini ama wapi mtu anatoka na kusema kuwa hakuna sababu ya kuwepo mambo hayo na kuwataka wananchi kuunga mkono maridhiano hayo kwa nguvu zao zote. 

Amesema kuwa, maendeleo makubwa yatapatikana iwapo patakuwa na umoja na amani. 

Amesisitiza kwamba, ipo haja ya kuendeleza maridhiano, kwani ilifika wakati watu walikuwa wakibaguana na kutaka hayo yote kuachwa nyuma na badala yake watu wafungue ukurasa mpya wapendane na wawe wamoja. 

Amesema kuwa, kazi ya kuhubiri amani na mshikamano ni ya watu wote na si viongozi wa siasa na dini peke yao. 

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amesema ipo haja ya kuutunza na kufundishwa elimu katika msikiti huo sambamba na kuutumia kwa kushauriana katika masuala ya kijamii zikiwemo changamoto za kijamii kama ilivyofanywa hapo siku za nyuma. 

Amesisitiza kwamba haitokuwa vyema kuwa na msikiti mzuri kama huo lakini maisha ya viongozi wa msikiti yakawa duni, kuwepo changamoto kwa jamii wakiwemo wajane hivyo, itakuwa si jambo la busara. 

Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa, milango yake iko wazi na kuwaahidi ushirikianao wake na kwa lolote watakalohitajia ushauri na mchango wake yuko tayari kutoa ushauri wake huku akieleza kwamba yuko tayari kuzifanyia kazi changamoto wanazozikabili wananchi wa Bumbwini. 

Amesema kuwa, hivi sasa Serikali inajipanga ili iweze kuleta maendeleo ambayo imewaahidi wananchi zikiwemo changamoto za wananchi wakiwemo wananachi wa Bumbwini na kueleza kwamba uundaji wa Serikali bado unaendelea. 

Mapema akimkaribisha Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Muhammed Mahmoud kwa niaba ya wananchi wa Bumbwini ametoa shukurani kwa ujio wa Rais Dkt. Mwinyi na kumueleza kuwa wataendelea kumuunga mkono.

Post a Comment

0 Comments