Rais Dkt. Mwinyi: Nina jambo, mniombee Mwenyenzi Mungu aniongoze

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaomba Waislamu kuendelea kumuunga mkono na kumuombea dua ili Mwenyezi Mungu amsaidie kwa yale yote ambayo amedhamiria kuwafanyia wananchi wa Zanzibar apate wepesi wa kuyatekeleza, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Alhaj Dkt. Hussein ameyasema hayo Desemba 4, 2020 huko Masjid Istiqama Shangani jijini Zanzibar wakati akitoa salamu kwa Waumini wa dini ya Kiislamu mara baada ya kumaliza sala ya Ijumaa.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dkt.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na kuagana na viongozi wa Masjid Istiqaama Shangani jijini Zanzibar, baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Masjid Istiqaama. (Picha na Ikulu).

Alhaj Dk. Hussein Mwinyi amesema kwamba, tayari ameanza kufanya kazi na ameona kasoro zilizopo na anataka kuzirekebisha, lakini anajua kwamba ni jambo la kawaida iwapo kasoro zitakapoanzwa kurekebishwa kuna mambo yatajitokeza.

Akiyataja mambo mawili yatakayotokea katika hatua hiyo, Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa ni pamoja na wengi watafurahia kwa sababu watanufaika na wachache hawatofurahia kwa sababu katika mfumo uliokuwa na makosa walikuwa wananufaika hivyo bila shaka watu hao hawatampenda.

Hivyo, Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi amewaomba Waislamu wamuombee dua ili aweze kutekeleza dhamira yake ya kuwatumikia wananchi wa Zanzibar.

Alhaj Dkt. Hussein amesema kuwa, aliomba nafasi ya Urais kwa dhamira moja tu ambayo ni kuwatumikia wananchi wa Zanzibar na kuwaletea maendeleo ambapo ndani yake havitokosa vikwazo hivyo alimuomba Mwenyezi Mungu kuviondoa ili yale yote yaliyo kwenye dhamira yake yaweze kutekelezwa.

Ametoa shukurani kwa kukamilisha uchaguzi kwa salama na amani na kumuomba Mwenyezi Mungu amani iliyopo izidi kudumu ili kuweza kuishi kwa amani na kufanya ibada kwa amani.

Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi ameeleza kuwa wakati wa kipindi cha uchaguzi alikwenda msikiti hapo na kuwaomba Waislamu na wananchi wote wa Zanzibar kwamba mara nyingi kipindi cha uchaguzi ndipo ambapo amani huvunjika na matatizo mengi hutokea kipindi kama hicho.

Hivyo, amewaomba wananchi wote waendelee kuilinda amani iliyokuwepo na kumuomba Mwenyezi Mungu kwa kujaalia kumalizika kwa uchaguzi mkuu kwa salama na amani na kusisitiza kwamba lililobaki hivi sasa ni kuendelea kuijenga nchi.

Alhaj Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa nchi hujengwa na wananchi wote na sio Serikali pekee yake na kutilia mkazo kwamba kila mtu akifanya wajibu wake pale alipo basi nchi itajengeka.

Ameongeza kuwa kila pale anapofanya uteuzi wa wasaidizi mbalimbali amekuwa akisisitiza kwamba kila mtu awajibike katika nafasi yake ya kazi.

Hivyo, Alhaj Dk. Hussein Mwinyi ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wote kila mtu alipo akiwa katika kazi ya Serikali, binafsi, ufugaji, mvuvi, ukulima kwani kila mtu akifanya jukumu lake ndipo maendeleo ya nchi hupatikana.Alisisitiza kuwa kwa upande wa Serikali anayoiongoza inafanya kila linalowezekana katika kuhakikisha yale yaliyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi na katika ahadi yanatekelezwa ambapo ili yatekelezwe kuna hitajika mambo mawili likiwemo la kwanza ni kuilinda amani iliyopo.

Aidha, alilitaja jambo la pili kuwa kuhakikisha kuwa kila mtu anwajibika katika nafasi yake ya kazi aliyonayo, kwani iwapo uwajibikaji utakuwepo na kila mtu atawajibika wakiwemo viongozi wa Serikali hakuna shaka kwamba yote yaliyoahidiwa kwa wananchi yatatekelezwa ikiwa ni pamoja na kuwaletea wananchi maendeleo.

Sambamba na hayo, Alhaj Dkt. Hussein amewashukuru na kuwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kudumisha amani iliyopo na kusisitiza kwamba hivi sasa na kwa upande wa Serikali iko tayari kuijenga nchi kwa mashirikiano ya wananchi wa Zanzibar na kumuomba MwenyeziMungu azidi kuleta baraka zake ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news