Rais Dkt.Mwinyi atumbua vigogo Zanzibar

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemsimamisha kazi Mkurugenzi Muendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii, Sabra Issa Machano na watendaji wengine kwa tuhuma za kuhusika na makosa mbalimbali katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya Serikali, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Zanzibar).
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akifuatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Katiba,Sheria (Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mhe.Haroun Ali Suleiman (wa pili kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), Mussa Haji Ali (wa pili kulia) Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Uchumi na Uwekezaji, Mhe.Mudrik Ramadhan Soraga (kulia) mara baada ya kumalizika kwa mkutano maalum na Wafanyakazi wa Idara hiyo leo uliofanyika Ofisi za Idara Victoria Garden jijini Zanzibar leo Desemba 23, 2020. (Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametoa kauli ya kuwasimamisha watendaji hao leo Desemba 23, 2020 wakati alipozungumza na viongozi na watendaji wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) katika ukumbi wa taasisi hiyo uliopo Victoria Garden, Vuga jijini hapa.

Watendaji wengine waliohusika na hatua hiyo ni pamoja na Ramadhani Abdalla Ali pamoja na watendaji wa Kamati nzima ya Uratibu wa mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) kutoka Wizara ya Fedha.

Amesema, amechukua uamuzi wa kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa ZSSF, Sabra Issa Machano pamoja Ramadhani Abdalla Ali kwa makosa ya kiutendaji katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Jumba la Treni lilopo Darajani. 

Amesema, ni dhahiri kuwa katika utekelezaji wa mradi huo taratibu zilikiukwa na hivyo akabinisha ulazima wa kufanyika uchunguzi, wakati ambapo watendaji hao wakiwa nje ya kazi.

Amesema, makosa dhidi yao hayatoi fursa ya wao kuendelea na kazi , hivyo ni vyema wakae pembeni kupisha uchunguzi na kusema Serikali itasimamia haki na kamwe hakuna mfanyakazi atakayeonewa dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

Aidha, amesema hafurahishwi na utekelezaji wa mradi wa ZUSP uliogharimu Dola Milioni 93, ambao ulikusudiwa kuondoa changamoto mbalimbali katika Manispaa.

Amesema, taarifa zilizopo zinaonyesha kuwepo makosa makubwa katika manunuzi pamoja na kufanyika udanganyifu juu ya kazi zilizoelezwa kufanyika wakati hazikufanyika.

Amesema, amelazimika kuisimamisha Kamati nzima ya Uratibu wa Mradi huo ili uchunguzi uweze kufanyika, wakati wafanyakzi hao wakiwa nje ya kazi zao.

Vile vile Dkt. Mwinyi ameagiza ZAECA kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya Mfanyakazi wa TRA, Haidar Mussa Maisara anayetuhumiwa kushusha kiwango cha kodi katika tukio la kuingizwa Bandarini kichwa cha Scania, sambamba na Kampuni ya KEVIS aliyoagiza ifanyiwe uchunguzi.

Amesema, mfanyakazi huyo alijenga dhamira ya kujihusisha na rushwa, ambapo kwa nyakati tofauti aliteremsha kiwango cha kodi hiyo hadi kufikia shilingi milioni tano, fedha ambazo haziendani na thamani halisi ya kodi iliyopaswa kulipwa, ambapo hatimae gari hilo lilitolewa usiku bila fedha hizo kulipwa.

Amesema, anasikitishwa na miradi mikubwa jinsi ilivyoghubikwa na matatizo makubwa kiasi ambacho haionyeshi thamani ya fedha zilizotumika na hivyo akaahidi kuchukua hatua mara moja dhidi ya wote waliokiuka kanuni za manunuzi.

Katika hatua nyingine Rais, Dkt. Mwinyi amesema, tangu Serikali ya Awamu ya Nane iingie madarakani imebaini kuwepo matatizo makubwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa, na hivyo akasisitiza dhamira ya Serikali ya kuchukua hatua madhubuti.

Aidha, amesema kuna miradi mingine inayoonesha dalili za kuwepo mianya ya rushwa na hivyo akaahidi kuifuatilia pamoja na kuhakikishia ZAECA kuwa serikali imefungua ukurasa mpya wa mapambano dhidi ya rushwa.

Mapema Waziri wa Nchi (OR) Katiba, Sheria, utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman amesema, kuna ushirikiano mkubwa wa kiutendaji kati ya ZAECA na wenzao wa Tanzania Bara (TAKUKURU) kutokana na vikao mbalimbali vilivyofanyika, na hivyo akaahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa lengo la kudumisha Muungano.

Alisema, akiwa Kiongozi wa Wizara, atasimamia kikamilifu kuona matukio ya rushwa na udhalilishaji yanamalizika kabisa hapa nchini.

Nae, Mkurugenzi Mkuu ZAECA, Mussa Haji Ali amesema, pamoja na taasisi hiyo kuasisiwa katika kipindi kifupi kilichopita, imeweza kupata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu yake makuu matatu.

Akigusia uchunguzi wa miradi mikubwa inayotokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya serikali, alisema ZAECA inaendelea kufanya uchunguzi katika miradi mbali mbali ikiwemo wa Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri na ukarabati wa jengo la Treni ambayo imebainika kuwepo harufu za rushwa.

Amesema, miradi mingine inayoendelea kufanyiwa uchunguzi ni Barabara ya Bububu-Mkokotoni Kaskazini Unguja pamoja na ile ya Ole – Kengeja inayoonekana kuwepo harufu ya rushwa katika suala la tathmini.

Aidha, ameitaja miradi mingine inayoendelea kufanyiwa uchunguzi kwa tuhuma za kuwepo mianya ya rushwa, kuwa ni pamoja na ujenzi wa Chuo cha Amali Vitongoji, Bandari ya Mangapwani, Soko la Matunda Kangani, Ujenzi wa kiwanda cha ushoni cha Idara Maalum, mradi wa kuendeleza vijana, ujenzi wa vituo vya Zimamoto Pemba, Kuimarisha majengo ya JKU Mtoni, Matengenezo kambi ya KVZ Pemba pamoja Chuo cha Mafunzo Wete.

Ameeleza kuwa, tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Nane, wananchi wamekuwa na imani kubwa na Serikali na hivyo wamekuwa wakisaidia katika utoaji wa taarifa.

Amemhakikishia Rais kuwa taasisi hiyo ina ushirikiano mzuri na taasisi za ndani na nje ya nchi pamoja na vyombo vyote vya uchunguzi ikiwemo TAKUKURU.

Akigusia changamoto, amesema taasisi hiyo inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa jengo lenye hadhi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi hivyo kuwa na tatizo katika upokeaji wa taarifa katika wilaya na mikoa.

Aidha, amesema taasisi inakabailiwa na changamoto ya vifaa mbalimbali vya utendaji pamoja na mafunzo kwa watendaji.     

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news