Rais Dkt.Mwinyi kuunda Tume Maalum ya Uchunguzi jengo la Beit el Ajaib

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kuunda Tume Maalum ya Uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha kuporomoka kwa sehemu ya jengo la Beit el Ajaib mwishoni mwa wiki iliyopita, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akitoa hutuba yake katika mkutano wa kujadili changamoto mbalimbali zinazopatika katika Mji Mkongwe wa Zanzibar na wadau wa Mji huo leo katika Ukumbi wa Idrissa Abdulwakil Kikwajuni jijini Zanzibar pamoja na sababu mbalimbali za kuporomoka kwa Jumba la Kihistoria la beit el Ajab wiki iliyopita na kusababisha maafa na hasara kwa Serikali ya Mapinduzi. (Picha na Ikulu).

Dkt.Mwinyi ameeleza hayo leo Desemba 28, 2020 katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil Kikwajuni jijini Zanzibar wakati alipokutana na wadau mbalimbali wa Mji mkongwe. 

Amesema, ipo haja ya kuunda Tume ya Uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali iliyotokea pamoja na kutafuta njia zitakazowezesha kuepuka majanga, sambamba na kuwepo uhifadhi bora wa mji huo. 

Amesema, ni jukumu la taasisi zilizopo Mji Mkongwe, ikiwemo Mamlaka ya Mji Mkongwe, Wakfu na Mali ya Amana pamoja na Shirika la Nyumba kushirikiana ikiwa ni hatua ya kuyatafutia ufumbuzi matatizo mbalimbali yanayokabili mji huo. 

Amesema, tume itakayoundwa itakuwa na jukumu la kuangalia sababu zilizosababisha kuporomoka kwa sehemu ya jengo hilo na nini kinahitaji kufanyika ili kuwepo uhifadhi bora wa mji huo, ukihusisha majengo yake. 
Aidha, amesema tume hiyo itaangalia changamozo zinazokabili taasisi zilizopewa mamlaka, akibainisha baadhi ya changamoto hizo hutokana na urasimu wa kiutendaji. 

Amesema, maeneo mengine yatakayopaswa kuangaliwa na Tume hiyo ni kuhusiana na weledi wa watendaji pamoja na muundo wa Bodi, huku akibainisha tume hiyo itafanya kazi kuambatana na hadidu rejea. 

“Lengo ni kutunza Mji na kuepusha maafa, mapendekezo yanapaswa kuwa ya muda mrefu, kati na mrefu ikizingatiwa gharama nyingi zinazohitajika,”amesema. 

Dkt. Mwinyi amesema, taarifa ya uchunguzi inapaswa kuainisha juu ya majengo yatakayohitaji kufungwa na wakaazi wake kuondolewa mara moja 

Ameeleza kuwa, Zanzibar imepoteza nembo muhimu ya Taifa na kusema wakati umefika wa kutizama ustawi wa mji mkongwe katika jicho la aina yake. 

Amesema, uchunguzi utakaofanywa haulengi kumtuhumu au kumuonea mtu, bali utazingatia haki na hivyo hatua zitachukuliwa pale itakapobainika kufanyika uzembe. 

Rais Dkt.Mwinyi, akitoa ufafanuazi wa baadhi ya mapendekezo amesema, katika mwelekeo wa kuwa na Mji Mkongwe uliohifadhika vyema, ni lazima kuwepo mfuko maalum wa Uhifadhi wa mji huo na kusema serikali itakuwa ya kwanza katika kuchangia, sambamba na kuwashajiisha wadau kufanya hivyo. 

“Serikali itaweka ‘seriousness’ katika uhifadhi wa mji mkongwe kwa kuwa na bajeti na wafanyakazi wenye taaluma pamoja na mfuko maalum, lakini pia naunga mkono suala la kuwa na ‘stone town day,” amesema. 

Aidha, amesema ni wakati muafaka wa kuangalia kwa makini utaratibu wa vyombo vya moto kuingia na kutoka katika eno la Mji Mkongwe. 
Ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Oman kwa utayari wake katika kusaidia uhifadhi wa mji Mkongwe wa Zanzibar. 

“Gharama za uhifadhi lazima zichukuliwe na Serikali kabla ya msaada, hivyo Serikali itakuwa mstari wa mbele katika kufanikisha jambo hilo, nawaomba wadau kufanya kila linalowezekana kutunza mji mkongwe, kwa kuwa ni chanzo kikuu cha mapato pale utakapohifadhiwa vyema,” amesema. 

Mapema, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Lela Mohamed Mussa pamoja na mambo mengine alisema katika tukio la kuporomoka kwa sehemu ya Jengo la Beit el Ajaib, mwishoni mw awiki iliyopita mafundi wanne walijeruhiwa na wengine wawili kufariki dunia. 

Aidha, Mkurugenzi, Mamlaka ya Mji Mkongwe Issa Sarboko Makarani, amesema miongoni mwa faida kubwa zinazotokana na Mji Mkongwe wa Zanzibar kuwepo katika Urithi wa Kimataifa ni kupata msaada wa matengenezo pale yanapotokezea maafa, ikiwemo kuporomoka kwa majengo yake. 

Amesema, Mamlaka ya Mji Mkongwe katika nyakatri zote imekuwa ikipata msaada mdogo wa kifedha kwa ajili ya kuyashughulikia majengo yake na ndio sababu ya kuporomoka kwa sehemu ya jingo la Beit al Ajaib na mengineyo, sambamba nakusema ukosefu mkubwa wa wafanyakazi wenye taaluma ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe kuwa ni changamoto kubwa inayoikabili mamlaka hiyo. 
Nao, wadau mbalimbali wa Mji Mkongwe wakichangia katika mkutano huo; waliishauri Bodi inayosimamia uhifadhi wa Mji Mkongwe kuwa na mainjinia wa kutosha ili kufanyakazi ya kuyakagua majengo mbali mbali yaliomo katika eneo hilo. 

Wamesema taarifa za uchakavu wa majengo ni vyema zikawa zinatumwa UNESCO kabla ili kuepuka majanga mbali mbali ikiwemo vifo. 

“Wizara inapaswa kuwa makini wakati wa kutafuta wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Mji Mkongwe, ili kuwa na watu wanaoendana na sifa na mahitaji halisi,”amesema Siti Abasi Ali. 

Aidha, wamesema Serikali inapaswa kusaidia katika usimamizi wa upigaji marufuku wa vyombo vya moto, (ikiwemo Bodaboda) kuingia katika eneo la Mji Mkongwe , ikiwa ni hatua ya kuimarisha usalama. 

Vile vile waliiomba serikali kuanzisha mfuko maalum (utakaoendeshwa kwa uwazi) katika dhana ya kuuendeleza uhifadhi pamoja na kutoza ada maalum kwa ajili ya kuchangia uhifadhi wa mji huo.

Wadau hao wamevitaka vyombo vya habari, hususan Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuwa na vipindi maalum vya kuutangaza Mji Mkongwe wa Zanzibar, wakati ambapo wameibua hoja kuwa wananchi wengi hawaelewi thamani ya Mji huo na utajiri mkubwa ulionao. 

Mkutano huo uliwashirikisha viongozi wa Kitaifa na wadau mbali mbali, akiwemo Mwakilishi Wa Balozi wa Oman, Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib haji, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mstahiki meya wa Jiji la Zanzibar Saleh Kinana, Viongozi wa Vikosi maalum vya Serikali ya Zanzibar, wawekezaji wa sekta ya utalii pamoja na wadau mbalimbali wa Mji Mkongwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news