RAIS MAGUFULI AAHIRISHA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA UHURU MWAKA HUU

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9, 2020 na ameelekeza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kununulia vifaa mbalimbali kwa ajili ya Hospitali ya Uhuru, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Desemba 3, 2020 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dkt. Magufuli ameagiza kiasi cha shilingi milioni 835,498,700 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe za maadhimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara zitumike kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya hospitali hiyo.

Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) zilizofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Amesema Rais Dkt. Magufuli ameagiza siku hiyo itumike kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii nchini.

Novemba 20, 2018, Rais Dkt. Magufuli aliagiza kiasi cha sh. milioni 995,182,000.00 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru, ambayo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 92.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa mwaka huu inasema; ‘Miaka 59 ya Uhuru na Miaka 58 ya Jamhuri: Tanzania yenye Uchumi Imara Itajengwa na Watanzania Wenyewe, Tufanye Kazi kwa Bidii, Uwajibikaji na Uadilifu.’

Waziri Mkuu amesema hadi kufikia sasa ujenzi wa hospitali hiyo ya Uhuru umegharimu shilingi bilioni 4.2. Januari 2019 wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya Simu ya Airtel Rais Dkt. Magufuli aliagiza kiasi cha shilingi 2,415,151,650.00 zilizotolewa na kampuni hiyo zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news