Rais Magufuli asali ibada ya Krismasi mjini Chamwino

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishiriki katika Misa Takatifu ya Krismasi katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu mkoani Dodoma leo Disemba 25, 2020.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Desemba, 2020 ameungana na Waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Imakulata, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma kusali Misa Takatifu ya Krismasi ambayo ni maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Baada ya Misa hiyo iliyoongozwa na Paroko wa Parokia hiyo Padre Paul Mapalala, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza na kuwatakia heri Watanzania wote kwa sikukuu ya Krismasi na amewataka kuendelea kumshukuru Mungu kwa miujiza na upendo mkubwa anaolitendea Taifa la Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipitisha kwa waumini kapu la sadaka aliposhiriki katika Misa Takatifu ya Krismasi katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu mkoani Dodoma leo Disemba 25, 2020.

Mhe. Rais Magufuli amesema upendo na miujiza ya Mungu kwa Tanzania inajidhihirisha katika kipindi hiki ambapo dunia inapita katika wakati mgumu wa janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19) ambapo maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha kila siku, lakini Tanzania imeepushwa na janga hilo na maisha ya Watanzania yanaendelea kama kawaida.

Amewaomba Watanzania wote waendelee kumshukuru na kumuomba Mungu aendelee kulilinda Taifa lao dhidi ya ugonjwa huo, na kuwaombea wananchi wa Mataifa mengine waepushwe na Korona.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimia waumini wenzie aliposhiriki katika Misa Takatifu ya Krismasi katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata Chamwino Ikulu mkoani Dodoma leo Disemba 25, 2020. (Picha zote na Ikulu).

Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa viongozi wa Mataifa mbalimbali duniani kukubali kumweka Mungu mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Korona badala ya kutegemea nguvu za binadamu pekee.

Pamoja na kuwatakia heri ya Krismasi, Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi za uzalishaji mali ili kuendelea kujenga Taifa lao pamoja na kuhakikisha wanamtanguliza Mungu kwa kila jambo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news