Rais Magufuli amtumbua Naibu Waziri wa Madini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amesema atafanya uteuzi wa Naibu Waziri wa Wizara ya Madini mwingine baada ya aliyemteua, Francis Ndulane Kumba kushindwa kuapa leo, anaripoti Mwandishi Diramakini (Dodoma).

Mheshimiwa Kumba ameonekana kumpa hasira Rais Dkt. Magufuli leo Desemba 9, 2020 Ikulu jijini Dodoma hadi kutamka wazi kuwa,"Tutateua mtu mwingine anayeweza kuapa vizuri.

Aidha, Kumba alikuwa miongoni mwa manaibu 23 ambao waliotakiwa kuapa lakini alikuwa akishindwa kutamka maneno na kutakiwa kukaa pembeni ili wenzake waendelee kuapa katika zoezi hilo.

”Wote nimewaangalia hata wewe uliyeshindwa kuapa na tutamteua Mtu mwingine ambaye ataweza kuapa vizuri, najua Waziri Mkuu ananiangalia kwa sababu Lindi wametoka yeye na huyu aliyeshindwa kuapa, sasa tutamteua mwingine na huyu tutacheki Degree yake vizuri.

“Nawapongeza Mawaziri 21 na Manaibu Waziri 22 walioapa, hongereni sana, mtakuwa na majukumu ya Ubunge na mengine kama Watendaji wa Serikali, kazi ya kuwateua ilikuwa ngumu, Wabunge zaidi ya 383 unachambua kutoka kwenye sample hiyo, hiyo ilikuwa Menu yangu,"amebainisha.

Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka katika Jiji la biashara Dar es Salaam, amemueleza Mwandishi Diramakini kuwa, hii ni ishara ya taa nyekundu kwa viongozi wengine ambao wamepewa dhamana na Mheshimiwa Rais kwenda kuwatumikia wananchi.

"Hii ni ishara ya taa nyekundu, maana yake ni kwamba, nafasi uliyopewa usipoweza kuitumikia kwa uadilifu na bidii kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla, unaondoka tena muda wowote, watambue tu kuwa, Mheshimiwa Rais Magufuli ni mtu wa vitendo si bla bla," ameeleza.

Post a Comment

0 Comments