Serikali yaagiza wastaafu walipwe mafao kwa wakati kupunguza malalamiko

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama ameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kulipa mafao ya wanachama wao kwa wakati ili kuepuka malalamiko yasiyo ya lazima, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini (Mwanza).
Waziri Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akihutubia wakati wa kufunga semina ya wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi ya Jamii (TSSA) walipokutana tarehe 19 Desemba, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Hotel ya Gold Crest Jijini Mwanza.Mkutano ulihudhuriwa na Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi mbalimbali wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko hiyo.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa kauli hiyo alipokuwa akifunga semina ya siku tatu iliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe wa Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi ya Jamii (TSSA) na kuhudhuriwa na Wenyeviti na Wajumbe wa Bodi mbalimbali wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko hiyo.

Waziri ameeleza, upo umuhimu wa kila mfuko kuona tija ya kulipa wanachama wao kwa wakati ili kuondokana na usumbufu unaoweza kujitokeza kwa wale wenye sifa za kulipwa na kusaidia wanachama hao kukidhi mahitaji yao kwa wakati mwafaka.

“Ni lazima kuhakikisha kuwa wanachama wanalipwa mafao yanayoendana na wakati ili kuwawezesha kukidhi matarajio yao bila kusahau wana mchango mkubwa katika mifuko yetu,"ameeleza Waziri.

Amefafanua kuwa, amekuwa akipokea malalamiko mengi kwa wastaafu kuhusu ucheleweshwaji wa mafao yao, hivyo kuonesha viashiria vya udhaifu kiutendaji na kuzielekeza mamlaka husika kutatua changamoto hiyo kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu.

Ameongezea kuwa, mifuko inawajibu mkubwa wa kuhakikisha Waajiri wanaandikishwa na wanalipa michango kwa wakati.Idadi ya Waajiri ambao hawalipi michango imeongezeka hususan makampuni ya Ulinzi.

“Mifuko ipunguze usumbufu usikuwa wa lazima kwa wanachama hasa baada ya kustaafu na kudai mafao, kwa mfano mwanachama anastaafu akiwa na miaka 60 anaanza kudaiwa nyaraka ambazo aliwasilisha wakati anasajiliwa, kama kuna mabadiliko ya taarifa zinatakiwa zifanyiwe kazi na maafisa matekelezo kabla mwanachama kustaafu,”amesisitiza Waziri Mhagama.

Aidha alieleza kuwa Azma ya Serikali ni kuona Watanzania wote wenye uwezo wa kufanyakazi wana andikishwa katika Mifuko ya Pensheni maana takwimu zinaonyesha bado kuna idadi kubwa ya wafanyakazi katika Sekta rasmi na isiyo Rasmi ambao bado hawajaandikishwa.

“Kwa kuangalia takwimu zilizopo, hadi sasa kuna jumla ya wafanyakazi walio andikishwa na kuchangia katika Mifuko kwa idadi ndogo, mfano mfuko wa NSSF wapo 543,889 na PSSSF ni 627,097 ambapo idadi hiyo ni sawa na 4.3% ya nguvu kazi (Labour Force). Hivyo kazi kubwa inatakiwa kufanyika hususan katika Sekta isiyo rasmi,”amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho la Mashirika ya Hifadhi ya Jamii (TSSA), Bw.William Erio amepongeza jitihada za Waziri katika kuratibu na kusimamia shughuli za mifuko iliyochini ya ofisi yake na kuahidi kutekeleza maagizo yake aliyoyatoa pamoja na kuhakikisha wanakuwa na mikakati thabiti ya kushiriki katika miradi ya kimkakati ya Serikali ili kuwa na tija katika Taifa.

Ameongezea kuwa, wanalenga kuhakikisha wanaboresha huduma zao kwa wanachama na kuwafikia kwa wakati ili kuendelea kunufaika na uwepo wa mifuko nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news