Serikali yataifisha Almasi ya Bilioni 61.9/- zilizokutwa uwanja wa ndege

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imetaifisha mzigo wa madini ya Almasi ambao ulikutwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere ukiwa unasafirishwa kwenda nchini Ubelgiji, wenye thamani ya sh.Bilioni 61, 970,625,864 fedha za Kitanzania, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Almasi iliyopo pichani haina uhusiano na iliyotoroshwa. (Picha na Maktaba).
 
Almasi hizo zina uzito wa carats wa 71,654.45 ambazo zilikuwa zinasafirishwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Uthaminishaji Almasi na Vito Tanzania (TANSORT), Archard Kakugendo na Mthamini Almas wa Serikali, Edward Rweyemamu.

Pia Mahakama hiyo, imewahukumu wathaminishaji hao ambao ni Kalugendo na Rweyemamu kulipa faini ya sh.milioni moja kila mmoja au kwenda jela miaka mitatu, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuisababishia Serikali hasara sh.Bilioni 61.9.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya baada ya washitakiwa kuandika barua kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Desemba 17, mwaka huu ya kuonyesha nia ya kuingia makubaliano ya kukiri kosa lao.

Awali kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, jopo la mawakili watatu wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Monica Mbogo, walidai shauri lilipelekwa kwa kutajwa na upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kwa Mamlaka ya Sheria ya Uhujumu Uchumi, DPP ameridhika kuwashitaki washitakiwa katika mahakama hiyo.

Pia Wakili wa Serikali, Jacqueline Nyantore, alidai kesi hii ni uhujumu Uchumi, hivyo DPP ameipa kibali Mahakama hiyo kesi kusikilizwa.

Akiwasomea shitaka alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na shitaka la kuisababishia Serikali hasara ambapo alidai Agosti 25 na 31, mwaka 2017 katika maeneo mbalimbali ya mikoa wa Dar es Salaam na Shinyanga, washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa wathamini wa Wizara ya Nishati na Madini walisababisha hasara ya dola za Kimarekani 29,509, 821.84, sawa na sh. bilioni 61.9 za Kitanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news