SERIKALI YAZINDUA MFUMO WA USIMAMIZI WA TAARIFA ZA WAJUMBE WA BODI ZA TAASISI ZA UMMA

Katika kuhakikisha taarifa mbalimbali za Wakala wa Serikali, taasisi na mashirika ya umma zinapatikana kwa wakati, Serikali imezindua matumizi ya mfumo mpya wa Usimamizi wa Taarifa za Wajumbe wa bodi za Taasisi za Umma pamoja na mfumo wa uchambuzi wa taarifa za fedha,anaripoti Victoria Kazinja (Diramakini) Morogoro.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora Dkt. Laurean Ndumbaro, katika uzinduzi wa mafunzo ya Mfumo wa kuhifadhi Taarifa za Wajumbe wa bodi za Taasisi na Mashirika ya Umma na Ufunguzi wa Mafunzo ya mfumo wa Uchambuzi wa Taarifa za fedha .

Dkt. Ndumbaro amesema utekelezaji wa mfumo huo unalenga kuimarisha usimamizi wa utendaji wa bodi na Menejimenti za serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Taasisi za Umma zinakuwa na Bodi za Wakurugenzi zilizo hai, na kupunguza watendaji wakuu wanaokaimu kwa muda mrefu.

‘‘Kutokuwepo kwa bodi ya Wakurugenzi katika Taasisi husababisha maamuzi mengi katika taasisi hiyo kukwama na kupelekea ucheleweshaji wa mambo mengi ya msingi kutofanyika kwa wakati’’ alisema Ndumbaro.

Kwa upande wake Msajili wa Hazina Athumani Mbuttuka, ameeleza kuwa mfumo huo utatumika katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mamlaka za Uteuzi wa Bodi za Wakurugenzi pamoja na Wakala za serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma katika usimamiaji wa masuala yote yanayohusu Bodi za Wakurugenzi.

Amesema mfumo huo umejengwa na wataalamu wa ndani ili kuhifadhi taarifa za uteuzi wa wajumbe wa bodi, wasifu wao, idadi ya Taasisi wanazohudumu, aina za ujumbe wao pamoja na kurahisisha utolewaji wa Taarifa za bodi kwa wakati.

‘‘Mfumo huu pia utasaidia upatikanaji wa taarifa za uhakika za wajumbe wa bodi na kwa wakati, ushiriki wao katika vikao na pia utapunguza urasimu wa ufuatiliaji wa uteuzi wa bodi pale inapomaliza muda wake, kuondoa changamoto ya Taasisi kutokuwa na bodi kwa muda mrefu, baadhi ya wajumbe kuteuliwa katika bodi zaidi ya tatu’’ aliongeza Mbuttuka.

Vilevile amesema Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea na juhudi za kuimarisha utendaji kwa njia ya kielektroniki ambapo imetengeneza na inaendelea na utengenezaji wa mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa ufuatiliaji na uchambuzi wa taarifa za fedha, mfumo wa Uandaaji wa bajeti na mfumo wa ufuatiliaji mali za serikali.

Hata hivyo jumla ya washiriki 708 kutoka katika Taasisi na mashirika ya umma 236 wanatarajiwa kujengewa uwezo wa kutumia mfumo huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news