Simai asisitiza umuhimu wa Chama cha Skauti Zanzibar

Makamu wa Rais wa Chama cha Skauti Tanzania, Simai Mohammed Said amesema uwepo wa Chama cha Skauti Zanzibar kutalisaidia Taifa kuwa na vijana wakakamavu pamoja na kuwa wazalendo wa nchi yao kutokana na mafunzo mbalimbali yanayotolewa ndani ya chama hicho, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza na viongozi wa Chama cha Skauti Zanzibar, ofisini kwake Mazizini Mjini Unguja, Simai amesema upo umuhimu wa kuboreshwa chama hicho Zanzibar ili kiweze kusikika na kutambulikana kwa lengo la kukuza vipaji vya watoto nchini.

Simai amesema kuwa, suala la upatikanaji wa eneo lao lina umuhimu kwani litasaidia kuwa kivutio kwa wageni na wenyeji pamoja na kuwashajiisha vijana kuweza kujiunga kwa kuweza kutanua wigo wa kuweza kujifunza masuala mbalimbali ya kikakamavu na kijamii.

Amesema atashirikiana na taasisi husika katika kuona wanapata eneo lao la kudumu ili waweze kuedelea kuwaelimisha vijana kuwa wajasiri na wazalendo wa nchi yao.

Simai ambaye pia ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar,amekitaka Chama cha Skauti Zanzibar kuishirikisha Wizara ya Elimu mipango mbalimbali ili kuangalia uwezekano wa kushirikiana katika mambo hayo kwa lengo la kuleta maendeleo katika nchi.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Zanzibar, Dkt Idrissa Muslim Hija amewataka Chama cha Skauti Zanzibar kuhakikisha wanapopanga mipango yao kuiwasilisha wizarani mapema ili kuepusha tatizo la upatikanaji wa fedha katika kutekeleza kazi zao.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu Msaidizi Skauti TSA Zanzibar, mwalimu Suleiman Ali Takdiir amesema, wana tatizo la ukosefu wa ofisi ambapo awali walikuwepo katika jengo la American Corner, lakini kwa sasa wamekuwa wakiazima ofisi tu kwa ajili ya kufanya shughuli zao.

Pia amesema wana tatizo la kifedha kwa ajili ya kushiriki Mkutano Mkuu wa mwaka ili kupata uwakilishi wa vijana kwa Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Dodoma, hivyo amemuomba Mhe Waziri kuliangalia suala hilo.

Katika hatua nyingine Chama cha Skauti Zanzibar katika kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi la kudumisha usafi wa mazingira nchini, kimemuhakiishia Mhe Waziri kuwa kipo tayari kujitolea kufuata agizo hilo katika maeneo mbalimbali ya Serikali na yasiyo ya Serikali ili kuleta haiba nzuri katika nchi.

Post a Comment

0 Comments