Stendi ya mikoani Mbezi Luis kuanza kutumika wiki ijayo

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhandisi Joseph Nyamhanga ametoa siku 14 kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha kituo cha mabasi yaendayo mkoani  na nchi jirani cha Mbezi Luis kinaanza kutumika ifikapo Desemba 20,2020, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza wakati wa zoezi la kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho Desemba 7, 2020 Mhandisi Nyamhanga amewataka kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa maeneo yaliyobaki ili kuanza kutoa huduma za usafiri kwa jamii.

Amefafanua kuwa,  kwa sasa kinachoendelea ni matengenezo madogomadogo ya umaliziaji wa majengo na miundombinu ya barabara ya kuingilia kwenye stendi hiyo, hivyo ni vyema wakaongeza kasi ya umaliziaji ili kituo hicho kianze kutumika kwa wakati.

Amesema kuwa, kazi ya ujenzi wa kituo hicho umekamilika kama ilivyoelekezwa Desemba Mosi, 2020 na msimamizi wa ujenzi ambaye ni kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam kilitoa hati ya awali ya kukamilika kwa ujenzi kwa mkandarasi ambapo sehemu kubwa imekamilika, hivyo kituo hicho kipo tayari kwa ajili ya kutoa huduma ya usafirishaji kwa jamii

Ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuhakikisha wanasimamia ujenzi huo kwa weledi na kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati uliopangwa usimamizi na kuhakikisha kuwa kituo hicho kinakamilika kwa wakati.

Mhandisi Nyamhanga ametoa maelekezo kwa uongozi huo kuhakikisha maandalizi muhimu yanafanyika kwa ajili ya kuanza kutoa huduma katika stendi hiyo ili huduma zinapoanza kutolewa kusiwepo na changamoto ambazo zinaweza kujitokeza

Aidha, amewaagiza Wakala wa Barabara (TANRODS) kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya kuingia kituoni hapo ili kuweza kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa jamii.

Vilevile, Mhandisi Nyamhanga ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kuhakikisha wanaandaa mpango kabambe wa eneo lililopo karibu na stendi ili kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza kwenye ujenzi wa mahoteli na nyumba za kulala wageni ili kuwarahisishia wasafiri maeneo ya kufikia wanapokuwa safarini..

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa,   Mhandisi Ngusa Julius amesema kuwa ujenzi wa barabara ya kuingia stendi ya mabasi itakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kuyawezesha magari kuingia na kutoka katika kituo hicho.

No comments

Powered by Blogger.