Tanzania yafungua ofisi ya Mwakilishi wa Heshima mjini Mumbai

Serikali ya Tanzania imefungua rasmi ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika Jiji la Mumbai,India katika hafla iliyofanyika jijini humo Desemba 4, 2020, anaripoti Mwandishi Maalum Diramakini.

Mumbai ni jiji kuu la biashara na viwanda nchini India (commercial and industrial hub) ambapo linachangia zaidi ya asilimia sita la pato la India na pia linachangia zaidi ya asilimia 25 ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani nchini India (25% of industrial output).
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda kwa pamoja na Mwakilishi wa Heshima Mteule wa Tanzania jijini Mumbai Bwana Nayan Patel wakisaini Mkataba wa Kazi wa kumwezesha Bwana Patel kuwa Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika mji huo. Mkataba huo ulisainiwa jijini Mumbai, India tarehe 04 Desemba 2020.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda na Bwana Nayan Patel wakibadilishana Mkataba wa Kazi wa kumwezesha Bwana Patel kuwa Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania katika mji wa Mumbai.

Aidha, Mumbai ni jiji mojawapo kati ya majiji kumi duniani, yanayoongoza kwa biashara, hususan katika mzunguko wa fedha duniani (global financial flow). Vilevile, Mumbai ni Jiji linaloongoza kuwa na mabilionea wengi nchini India, ambapo linashika nafasi ya 9 kuwa na mabilionea wengi duniani.

Kadhalika, shughuli za biashara na huduma za kifedha katika Jiji hilo lenye watu zaidi ya milioni 20 zinachangia mzunguko wa fedha katika uchumi wa India kwa zaidi ya asilimia 70.
Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini Mumbai Bwana Nayan Patel akihutubia katika hafla ya ufunguzi rasmi wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini humo iliyofanyika tarehe 04 Desemba 2020.

Ni kutokana na umuhimu wa Jiji hilo, Serikali iliamua kusogeza karibu huduma za kikonseli, biashara, uwekezaji, utalii na mengineyo kwa kuwa na Mwakilishi wa Heshima atakayeratibu shughuli hizo kwa karibu. Ikumbukwe India ni nchi kubwa yenye uchumi mkubwa na idadi kubwa ya watu duniani wanaofikia bilioni 1.2. Hivyo, si rahisi kwa nchi zenye uwakilishi mjini New Delhi kuweza kuhudumia kwa ukamilifu nchini India bila kuwa na ofisi za aina hii.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda alielezea juu ya umuhimu wa ofisi ya Mwakilishi wa Heshima jijini Mumbai kuwa itasaidia kutoa huduma za Kikonseli kwa karibu zaidi na pia itasaidia zaidi kuvutia na kutangaza fursa mbalimbali za biashara, uwekezaji zilizopo nchini, kutafuta masoko ya bidhaa za kilimo na viwanda vya Tanzania pamoja na vivutio mbalimbali vya utalii wa Tanzania ili kukuza sekta ya utalii nchini.
Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akitoa hotuba kumpongeza Bwana Patel kwa kukubali kuiwakilisha Tanzania jijini Mumbai na kumtaka kuiwakilisha vema nchi
Balozi wa Tamzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda na Mwakilishi wa Heshima wa Tanzania Jijini Mumbai Bwana Nayan Patel wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wageni walioshriki halfla ya uwekaji saini wa Mkataba wa Kazi wa Mwakilishi wa Heshima.

Aidha, Balozi Luvanda alieleza kuwa ofisi hiyo itachangia katika kukuza biashara zaidi kati ya Jiji la Dar es Salaam na Mumbai kufuatia kuimarishwa kwa huduma za usafiri wa anga baada ya Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania) kuanza safari zake za ndege za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai tangu mwezi Julai 2019. Vilevile, majiji haya yanaunganishwa na bandari kuu muhimu ambazo ni Bandari ya Dar es Salaam, kwa upande wa Tanzania, na Bandari ya Mumbai, kwa upande wa India.

Bwana Nayan Patel, ni raia wa India na mfanyabiashara mwenye mtaji mkubwa jijini Mumbai na amekwishaanza rasmi kazi ya Uwakilishi wa Heshima baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kidiplomasia. 

Bwana Patel aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa heshima kubwa ya kuiwakilisha Tanzania jijini Mumbai na maeneo mengine ya jirani na akaahidi kuitendea haki nafasi hiyo kadri atakavyoweza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news