TCAA ,TAA waruhusu ATCL kuanza safari za ndege Geita

Shirika la Ndege nchini (ATCL) limetangaza kuanza safari zake za ndege za abiria kwa kuruka na kutua katika Uwanja wa Ndege wa Geita hivi karibuni,baada ya kusaini mkataba wa makubaliano katika kikao cha utayari wilayani Chato Desemba 8, mwaka huu baina ya Mamlaka ya Anga (TCAA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege (TAA),anaripoti Robert Kalokola (Diramakini) Geita.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi (wa pili kulia) akifafanua jambo baada ya kikao cha utayari wa kuanza kurusha ndege za abiria katika kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Matindi amesema, ATCL imepeleka ndege zake katika mkoa huo baada ya kuona mkoa huo una uchumi mzuri unaotokana na uchimbaji wa madini ambao unawezesha shirika hilo kupata abiria wa kutosha.

Amesema, baada wadau wa usafiri wa anga kuthibitishia shirika hilo kuwa linaweza kuanza kutumia kiwanja hicho cha ndege kusafirisha abairia,ATCL kuanzia sasa itaanza safari zake katika kiwanja hicho.

Mkaguzi wa viwanja vya ndege kutoka TCCA, Mhandisi Benard Kavishe amesema kuwa, kuanza kwa safari za ndege katika uwanja huo kutafungua ajira za moja kwa moja 400 na nyingine zisiyo za moja kwa moja.

Mhandisi Benard Kavishe amesema hayo baada baada ya ukaguzi wa kiwanja hicho cha ndege cha Mkoa wa Geita na kuridhika na ujenzi wake na kwamba uko tayari kwa ajili ya matumizi.
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Geita, Mhandisi Haroun Senkuku akitoa taarifa ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Mkoa wa Geita. (Picha na Robert Kalokola/Diramakini).

Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Mkoa wa Geita, Mhandisi Haroun Senkuku amesema, kiwanja hicho kimejengwa kwa gharama ya sh.Bilioni 58 na kimekamilika kwa asilimia 95.

Mhandisi Senkuku ametaja baadhi ya maeneo yaliyokamilika kujengwa ni pamoja na eneo la njia ya kukimbilia ndege(runway),maegesho,eneo la usalama na eneo la abiria.

Amesema, baadhi ya maeneo ambayo hajajengwa ni pamoja na uzio,jengo la abiria na jengo la taasisi mbalimbali.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel akizungumza katika kikao cha utayari wa kuanza kusafirisha abiria katika kiwanja Cha ndege cha Geita. ( Robert Kalokola).

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema kuwa, kiwanja hicho kitasaidia wawekezaji hasa kwenye madini kuja mkoa wa Geita kufanya shughuli zake.

Amesema kuwa, serikali itahakikisha usalama wa kutosha na kuhakikisha kiwanja hicho hakitumiki kutorosha madini na madawa ya kulevya.

Taasisi tatu ambazo ni mamlaka ya anga nchini, mamlaka ya usimamizi wa viwanja vya ndege na shirika la ndege zimekutana katika kikao cha pamoja cha utayari kwa ajili ya kusaini makubaliano ya kuruhusu ATCL kuanza kutoa huduma za kusafirisha abiria .

Post a Comment

0 Comments