Usichokijua kuhusu Desemba 26 ya usiku wa Tamasha la Muziki la Serengeti

Usiku wa Desemba 26, 2020 utakuwa ni mwendelezo wa matamasha ya kufunga mwaka yanayowahusisha wasanii na wananchi katika kuburudika na kusherehea mafanikio ya kazi za Sanaa nchini,anaripoti Eleuteri Mangi (WHUSM) Dar es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akitangaza kukamilika kwa maandalizi ya Tamasha la Muziki la Serengeti ambalo litakalofanyika Desemba 26, 2020 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Tamasha la Muziki la Serengeti limekuja kunogesha Siku ya kufungua zawadi ambapo linahusisha wasanii kwa lengo la kuwaletea watanzania furaha, amani, utulivu, utu wema na udugu ambavyo ni tunu za taifa ambazo ni nyenzo za kulisaidia taifa na Watanzania kufikia maendeleo endelevu. 

Siku hiyo itawafanya watanzania kuwa na siku yenye bashasha kufurahia kazi za wasanii wetu na kuenzi kazi zao ambazo kila mara zimekuwa kioo cha nchi yetu na kimataifa. Ufundi wao wa kazi ya sanaa umekuwa msingi adhimu wa kumfanya mtanzania na wapenzi wa muziki wa Bongo fleva kufikisha fikra au mawazo ambayo yanasaidia kuelimisha, kuonya, kuburudisha na kufundisha jamii. 

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo yenye dhamana ya kusimamia sekta ya Sanaa ipo mstari wa mbele kwa kushirikiana na wadau wengine kuratibu, kusimamia na kutekeleza tamasha la Serengeti Music and Art Festival ambalo litakalofanyika Desemba 26, 2020 katika Uwanja wa Uhuru. 

Kutokana na umuhimu wake, wamejitokeza wadau kadhaa ambao wameunga mkono wazo la tamasha ambalo linalenga kuwaleta pamoja na kuwaunganisha wasanii mbalimbali kupitia kazi zao za sanaa. 

Wadau hao ni kampuni ya Multichoice, redio EFM, Clouds media, redio 5, Peramiho DJ’s, Global TV, Elsewedy Electric, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Chanel 10, Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Shirika la Mawasiliano la Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) pamoja na benki ya NMB, CRDB. 

Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amewathibitishia Watanzania tamasha hilo limekuja muda mwafaka na ni tamasha la kipekee ambalo litawaleta pamoja wasanii na wananchi. 

Uamuzi wa kufanyika kwa tamasha hilo ni taswira ya uamuzi mahiri alioutangaza Dkt. Abbasi Desemba 02, 2020 Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wake na wasanii wa tasnia ya filamu ambapo alisisitiza kuwa siku hiyo itakuwa ni maalum kwa ajili ya kusherekea sanaa za Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wasanii wakati wa kutangaza kukamilika kwa maandalizi ya Tamasha la Muziki la Serengeti ambalo litakalofanyika Desemba 26, 2020 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Hakika huu ni mwanzo mpya katika sekta ya Sanaa kuwa na tamasha ambalo linawaleta pamoja wasanii wakongwe na chipukizi ili waweze kubadilisha uzoefu hatua ambayo imekuwa na mwitikio mkubwa wa wasanii ambao wamelipokea kwa furaha na kuthibitisha ushiriki wao. 

Hadi sasa zaidi ya Wasanii 60 wamethibitisha kushiriki tamasha hilo wakiwemo wasanii wa muziki wa kizazi Kipya (Bongo Fleva) wa sasa na wazamani, wamuziki wa nyimbo za Injili, singeli, sanaa za maonesho kama maigizo na sarakasi na pia filamu fupi za Bongo Movie. 

Idadi hiyo ya wasanii inaleta taswira ya ushirikiano, Amani na upendo miongoni mwao. Wasanii hao ni pamoja na Sholo Mwamba, Nandy, Mrisho Mpoto, Christina Shusho, Kala Jeremiah, THT, Aslay, Becka Fleva, Shilole, Chege, Snura, Jesca Mshama, Dogo Janja, Dulla Makabila, Baby Madaha, Stamina, Meja Kunta, GoodLuck Gozbeth, Linah, Barnaba, Young Dee, Mabantu, Msechu, Pam D, Msami, Madee, Whouz, Fid Q, Weusi, Maarifa, Rapcha, MoniCentralZone, Baddest 47 and Dully Sykes 

Huku wasanii wanaowakilisha Bongo Fleva wa awali ni Inspector Haroon, Matonya, Z Anton, Tunda Man, Kassim Mganga, TID, Feruz, Soggy Dogg, Chid Benz, Mb Dog, Wateule, Wagosi wa Kaya, East Coast Team, TMK wanaume na Mtafya na Nini 

Kufanyika kwa tamasha hilo ni utekelezaji wa sera ya kitaifa ya maendeleo ya Sanaa hatua inayosaidia kusisitiza matumizi ya maadili ya kitaifa katika shughuli za muziki, sanaa za maonesho na ubunifu kwa jumla. 

Tamasha hilo litaanza Saa 08:00 Mchana katika Uwanja wa Uhuru mpaka Alfajiri na kiingilio ni Tsh. Shilingi 5,000 na fedha hizo zinalipwa kwa mfumo wa N-CARD ambazo zinapatikana katika maeneo mbalimbali ikiwemo Maduka ya Sunderland Sports Wear-Mtaa wa Kariakoo/Nyamwezi, Merere Sports Wear - Kariakoo Mkabala na Big Bon Msimbazi, Maduka ya Shafii Dauda-Sinza Makaburini na Tabata, 

Maduka ya Vunja Bei-Sinza Madukani, Sinza Makaburini na Kinondoni pamoja na Uwanja wa Uhuru ambapo kadi hizi zitakuwa zikiuzwa muda wote kabla na siku hiyo ya tamasha. Lipia tiketi yako sasa kupitia huduma za kifedha za M-Pesa, Tigo Pesa, Airtel Money pamoja na T-Pesa. 

Mapato na matokeo ya tamasha hilo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuendeleza mifumo ya kutambua wasanii katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya sanaa. 

Aidha, Dkt. Abbasi ameongeza kuwa burudani itaendelea Desemba 27, 2020 katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ambalo linahusu kazi mbalimbali za Sanaa ikiwemo uchongaji, uchoraji, burudani za asili za sarakasi na ngoma. Tamasha hilo halitakuwa na kiingilio ambapo watu wote wanakaribishwa kufurahia ubunifu na kazi za Sanaa za maonesho.

Post a Comment

0 Comments