WANAOFANYA MAPENZI NA WASICHANA WENYE UMRI MDOGO WAONYWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa Majaliwa ametoa onyo kali kwa wanaofanya mapenzi (ngono) na wasichana wenye umri mdogo, hali inayosababisha kuwaharibia malengo yao ya baadae, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Majaliwa ameyasema hayo leo Desemba 2,2020 wakati akiwahutubia wananchi kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Mandela Moshi, Mkoani Kilimanjaro yenye kauli mbiu ya "Mshikamano wa kimataifa, Tujumuike Pamoja".

"Nataka niwakumbushe na kutoa tahadhari kwa wale watu wazima mnaofanya mapenzi na vija wadogo wa kike, ole wenu, ole wenu, ole wenu," ameyasema Majaliwa. 

Amesema kuwa, takwimu za maambukizi mapya ya VVU zinaonesha kwamba asilimia 40 ya maambukizi hutokea kwa vijana na katika hao asilimia 80 ni vijana wa kike, huku akiweka wazi kuwa, vijana ni kundi linalokabiliwa na changamoto ya maambukizi mapya ya VVU nchini.

Ameendelea kusema, kundi la vijana na hasa wa kike lipo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi mapya, huku akidai uchambuzi wa kimazingira kuhusu takwimu hizi unaonesha kuwa sababu za vijana kuwa katika hatari ya maambukizi mapya ya VVU ni pamoja na kuanza ngono katika umri mdogo, vijana wadogo wa kike kuwa na mahusiano ya kingono na wanaume wenye umri mkubwa matumizi yasiyo sahihi na endelevu ya mipira ya kike na kiume.

Aidha,Majaliwa, ametoa wito kwa vijana kujitambua na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, huku akiwakumbusha kuwa vijana ndio nguvu kazi ya Taifa, na kuwataka wale wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao. 

"Natoa wito kwa vijana kujitambua na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa kuwa ninyi ni nguvu kazi na Taifa linawategemea. Na wale wanaoishi na VVU waendelee kutumia dawa za ARV kwa ufuasi sahihi bila kuacha ili kufubaza VVU na kuimarisha afya zao,"amesema Majaliwa. 

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amesema kuwa, Tanzania na Dunia kwa ujumla imepiga hatua kubwa katika jitihada za kukabiliana na janga la VVU na UKIMWI.

Ameendelea kusema kuwa, kama nchi inavoelekea kufikia malengo ya Tisini Tatu, changamoto, na vipaumbele vimeendelea kubadilika kutokana na mafanikio ya mwitikio wa mapambano.

Takwimu zinaonesha kuwa wanaume, watoto, vijana wanaopevuka na vijana wadogo, na watu wanaofanya tabia hatarishi, wako nyuma kutambua hali zao, ufuasi hafifu wa tiba, na ufubazaji wa VVU usioridhisha. 

Hata hivyo, Prof. Mabula Mchembe amesema kuwa, Serikali inaendelea na jukumu la kutafiti, kuandika na kusambaza taarifa za kitaalamu zinazochambua na kutoa masuluhisho ya changamoto zitazotumika kuhuisha sera, miongozo na taratibu za huduma na afua za VVU na UKIMWI. 

"Tunalo jukumu sasa, la kutafiti, kuandika na kusambaza taarifa za kitaalamu zinazochambua na kutoa masuluhisho ya changamoto hizi ili sasa yatumike kuhuisha sera, miongozo na taratibu za huduma na afua za VVU na UKIMWI," amesema Prof. Mchembe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news