Wasanii waliotwaa tuzo AEUSA, Oscars,Serengeti Boys wapongezwa

Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa amewapongeza wasanii wa Muziki wa Bongo Fleva waliofanya vizuri kwenye tuzo za AEUSA, msanii bora wa filamu za Oscars pamoja na timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Serengeti Boys ambao wamefuzu kushiriki mashindano ya AFCON U-17 yatakayofanyika mwaka 2021 nchini Morocco, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Msanii Nasibu Abdul (Diamond Platnumz) pamoja na Faustina Mfinanga (Nandy) wameshinda tuzo ya African Entertainment Award USA (AEUSA) katika kipengele cha wasanii bora wa Afrika kwa upande wa wanaume na wanawake huku Raymond Mwakyusa (Rayvanny) amepongezwa kwa kushinda kipengele cha msanii bora wa Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini. 

Aidha, katika mchezo wa filamu mwadada Shahista Alidina (Shyakaa) ameshinda tuzo ya msanii bora wa filamu za Oscars katika mashindano yaliyofanyika Desemba 18, 2020 Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

“Taifa na Watanzania wote tunajivunia mafanikio ya vijana wetu kwa tuzo walizopata katika sekta ya sanaa pamoja na ushindi wa Serengeti Boys katika sekta ya michezo. Hii ni hatua nzuri ya kuitangaza nchi yetu kwa kupeperusha vyema bendera ya Taifa letu katika medani ya kimataifa,”amesisitiza Mhe.Bashungwa.

Bashungwa amewapongeza vijana wa timu ya Taifa chini ya Umri wa miaka 17 Serengeti Boys kwa kufanikiwa kuingia fainali ya mashindano ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) U-17 ambapo wameitoa timu ya Taifa ya Ethiopia kwa kuifunga kwa jumla ya magoli 4-3.

Amesema, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa wadau wa sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuhakikisha taifa linasonga mbele katika medani za kimataifa.

Post a Comment

0 Comments