Waturuki wavutiwa kuwekeza Tanzania

Wawekezaji kutoka nchini Uturuki wamewasili nchini Tanzania hivi karibuni kwa ajili ya kujionea fursa za uwekezaji na biashara zilizopo nchini ili waweze kuwekeza na kukuza Diplomasia ya Uchumi baina ya mataifa hayo, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo alithibisha kuwasili kwa wawekezaji hao wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki ya Compass Partners jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa wawekezaji watano kati ya kumi wamefika nchini na kujumika na Waturuki wengine wanaofanya biashara zao hapa nchini. 
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo akiongea na wanahabari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki ya Compass Partners jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

"Wawekezaji hawa kutoka Uturuki wamekuja na wamefungua taasisi yao inayojulikana kwa jina la Compass Partners ili kuendeleza biashara na tunaamini kwa kutekeleza biashara hii tunaenda kuendeleza uchumi wa Tanzania na kutengeneza ajira kwa watanzania,"amesema Prof. Kiondo. 

Prof. Kiondo ameongeza kuwa, hatua ya kwanza wawekezaji hao wameleta bidhaa mbalimbali ili watanzania wazione, hatua ya pili itakuwa ni uwekezaji wa kiwanda hapa nchini kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa bidhaa ambazo zitauzwa hapa nchini. 
Kaimu Balozi wa Uturiki hapa Nchini, Mhe. Onur Yah akiongea na wanahabari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki ya Compass Partners jijini Dar es Salaam.

Aidha, kwa upande wa bidha zinazozalishwa hapa nchini ambazo zina fursa ya kuuzwa Uturuki ni pamoja na chai, pamba, tumbaku na kahawa bidhaa hizi zote zina soko kubwa sana nchini Uturuki. 

"Tunazalisha tani 350,000 za pamba lakini tunaweza kuchakata asilimia 15 tu, hivyo tumepata tayari mwekezaji ambaye atawekeza katika kiwanda cha nguo mkoani Simiyu ili kuongeza thamani ya bidhaa ya pamba hapa nchini,"amesema. 

Balozi, Prof. Kiondo ametoa wito kwa Watanzania kuanza kuchangamkia fursa hizo za biashara ili waweze kuongeza kipato na kuongeza biashara zao. 

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Uturiki hapa Nchini, Mhe. Onur Yah amesema kuwa biashara kati ya Tanzania na Uturiki imekuwa ikiimarika kila wakati kwani Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza na kufanya biashara.
Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Mhe. Prof. Elizabeth Kiondo pamoja na Kaimu Balozi wa Uturiki hapa Nchini, Mhe. Onur Yah wakikata utepe wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Waturiki ya Compass Partners jijini Dar es Salaam.

"Kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali ni imani yangu kuwa tutaendelea kukuza na kuimarisha uhusiano wetu wa kidiplomasia,"amesema Mhe. Yah. 

Aidha, amewataka Waturuki na Watanzania kutumia fursa za biashara zinazopatikana baina ya mataifa hayo ili kufanya biashara na kukuza uchumi wao. 

Ushirikiano wa Tanzania na Uturuki ni wa muda mrefu, pamoja na mambo mengine uhusiano huo umekuwa ukijikita zaidi katika kuendeleza uwekezaji wa viwanda, elimu na utalii hasa katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Uturuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news