Waziri Haroun Ali Suleiman atoa maelekezo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu

Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wametakiwa kuwajibika na kuwa wazalendo katika majukumu yao ili kuleta ufanisi zaidi katika kazi zao za kila siku, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman ameyasema hayo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Mazizini jijini Zanzibar wakati wa akimalizia ziara ya kutembelea taasisi zilizopo katika wizara yake. 

Amesema, iwapo wafanyakazi watasimamia majukumu yao kwa uadilifu na uwajibikaji wataweza kufikia lengo na kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza katika utendaji wa kazi kwa kuzingatia sheria,taratibu na kanuni za kazi.

Amesema kuwa, Zanzibar itajengwa na Wazanzibari wenyewe kwa kuthamini kazi walizopewa hivyo kuna wajibu wa kila mfanyakazi kuheshimu sheria na kanuni za uwajibikaji ili kufikia lengo la Rais kwa kutaka kuinyanyua Zanzibar kiuchumi.

“Zanzibar tuhakikishe tunaitetea na kuijenga kwa nguvu zetu zote hivyo kila mmoja awajibike katika eneo lake kazi alilopangiwa na afike na kuondoka kwa wakati ulioweka na sheria za utumishi,”amesema Waziri. 

 Pia amewahakikishia wafanyakazi hao kuwa atasimamia ipasavyo kuhakikisha wanapata nafasi ya kutosha kwa kuongeza ghorofa mbili na kwa upande wa Pemba watajenga jengo la ofisi yenye nafasi ya kutosha hivyo amewataka waandae michoro kwa ajili ya ujenzi huo huku akisisitiza mafunzo kwa wafanyakazi.

Nae Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Dkt.Mwinyi Talib Haji ameahidi kusimamia maslahi ya wafanyakazi wake na kuwaendeleza kimasomo ili kuondoa malalamiko kwa baadhi ya wafanyakazi hao. 

Amesema, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ina rasilimali watu wa kutosha hivyo kwa umoja wao watajitahidi kuyatekeleza yale ambayo yanategemewa kisheria na kikatiba ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Akitoa taarifa fupi Mkurugenzi Mipango Uendeshaji Rasilimali Watu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Hamisa Mmanga Makame amesema kuwa ofisi inahitaji Wakili dhamana ambae atakuwa Msimamizi Mkuu wa Ofisi kwa upande wa Pemba.

Amesema kuwa, katika kutekeleza majukumu yake idara imeshughulikia na kuandaa kanuni 13 zinazotokana na sheria tofauti kwa lengo la kuzifanya sheria hizo ziweze kutekelezeka kwa ufanisi zaidi.

Hata hivyo, amesema kuwa kesi 46 zimesimamiwa kwa kipindi cha Julai hadi Septemba na kati ya kesi hizo tayari kesi tano zimeshatolewa hukumu, na kesi 41 zinaendelea ambapo kwa Unguja kesi 34 zimesimamiwa na kwa upande wa Pemba kesi saba zimesimamiwa tayari.

Post a Comment

0 Comments