Waziri Jafo amsimamisha kazi Mkurugenzi Geita Mji

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR -Tamisemi), Mhe. Selemani Jafo amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mji wa Geita, Bw. Modest Joseph Apolinary kupisha uchunguzi kufuatia ununuzi wa gari yenye thamani ya shilingi millioni 400, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akiongea leo na Menejimenti ya Ofisi ya Rais- TAMISEMI jijini Dodoma, Waziri Jafo amesema kuwa, mara baada ya Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Madiwani kuvunjwa majukumu yote yalikasimishwa kwa wakurugenzi na kupelekea baadhi ya Halmashauri kutumia mwanya huo kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.

“Halmashauri ya Mji wa Geita katika kipindi hicho ambacho baraza la madiwani halipo waliweza kununua gari lenye thamani ya shilingi milioni 400, jambo hili halikubaliki kwa kuwa ni matumizi mabaya ya fedha za umma,”amesisitiza Waziri Jafo. 

Ameendelea kufafanua kuwa Geita wana fursa nyingi za madini,  lakini wamenunua gari moja kwa gharama hiyo wakati katika eneo hilo kunauhitaji mkubwa wa vituo vya afya, madawati na vyumba vya madarasa, jambo hili ni kinyume na maadili ya kiutumishi na linarudisha nyuma juhudi za Serikali za kutoa huduma bora kwa wananchi.

Waziri Jafo amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhandisi Joseph Nyamhanga kuunda timu ya uchunguzi ambayo itachunguza kwa kina matumizi ya fedha katika Halmashauri ya Mji Geita.

Pia amemuagiza Katibu Mkuu huyo kufanya uchunguzi zaidi kwa mwanasheria na mweka hazina wa halmashauri hiyo wakiwa ni washauri wakuu wa Mkurugenzi ni kwa jinsi gani waliweza kutimiza majukumu yao kikamilifu katika kushauri kuhusu ununuzi wa gari hilo. 

Sambamba na hilo Waziri Jafo amekiagiza Kitengo cha Ukaguzi Ofisi ya Rais-TAMISEMI kufanya uchunguzi na ufuatiliaji kwa halmashauri nyingine zenye kutiliwa shaka kama zilienda kinyume cha taratibu ya matumizi ya fedha.

Aidha,amemuagiza Katibu Mkuu kuunda timu itakayochunguza Ofisi ya Mkurugenzi, Manunuzi, Mwekahazina na Wakuu wa vitengo wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda juu ya tuhuma zinazotolewa na wananchi kuhusu matumizi mabaya ya fedha katika halmashauri hiyo, ili endapoitabainika kuwa ni kweli hatua sitahiki zitachukuliwa kwa wahusika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news