Waziri Mkuu aipa wiki mbili TPA, Bandari ianze kufanya kazi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipa wiki mbili kuanzia Desemba 18, 2020 Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ihakikishe kwamba ifikapo Januari Mosi mwakani Bandari ya kimkakati ya Kagunga iliyoko katika Kata ya Kagunga wilayani Kigoma iwe imeanza kutoa huduma. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Fred John Liundi (kulia) Bandari Tanzania na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobia Andengenye wakati aliopowasili kwenye Bandari ya Kagunga mkoani Kigoma. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Leo nimekuja hapa kuona bandari, hii bandari ilikamilika mwaka 2017 imekaa tu, nyumba zimejaa popo tu na mle ndani kumejaa takataka na mmefagia jana baada ya kusikia mimi nakuja, hovyo kabisa nawauliza hapa wanajikanyaga tu tuna mtumishi hapa hakuna mtumishi amekuja jana badaa ya kusikia nakuja hovyo kabisa hawa.” 

Alitoa agizo hilo baada ya kukagua mradi wa bandari ya Kagunga iliyopo kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika, wilayani Kigoma. Waziri Mkuu amechukizwa na kitendo cha bandari hiyo kushindwa kutoa huduma licha ya kuwa imekamilika. 

Waziri Mkuu alisema mbali na bandari hiyo ya Kagunga kuanza kazi Januari Mosi, 2021, pia ameagiza soko la kisasa la Kagunga nalo lianze kazi siku hiyohiyo ili kuwawezesha wananchi wa Kagunga waanze kufanya biashara na kuinua kipato chao. 

Pia, Waziri Mkuu alishangwaza na kuchukizwa na kitendo cha Meneja wa Bandari kutoka Makao Makuu ya TPA ambaye hajawahi kufika katika bandari hiyo na haijui. “Kama kweli wewe ni Meneja wa Bandari Tanzania bandari zako huzijui na unamiaka chungunzima unafanya kazi gani, hovyo kabisa.” 

Waziri Mkuu alisema mradi wa ujenzi wa bandari hiyo ulikamilika 2017 ukihusisha ujenzi wa jengo la abiria pamoja na la mizigo, nyumba ya kuishi mtumishi na jengo maalumu lakini hakuna mtumishi katika bandari hiyo ambayo ujenzi wake uligharimu shilingi bilioni 3.8. 

“…Tarehe moja ya mwezi wa kwanza mwaka 2021 nataka bandari hii ianze kazi, nenda mkajipange. Hapa hakuna mtumishi hamisha watumishi kama wapo Dar es Salaam, kama wapo Kigoma leta watumishi hapa wawatumikie wananchi kwenye bandari hii.” 

Aliwaagiza watendaji wa TPA waruhusu meli na boti za watu binafsi zifanyekazi ya kutoa huduma katika bandari hiyo ili kuwawezesha wananchi kusafiri na kusafirisha mizigo kwa urahisi. Amesema Serikali inataka majengo hayo yatumike kama ilivyokusudiwa. “Hizi fedha za Watanzania shilingi bilioni 3.8 watu wanafanya nazo mchezo tu, nataka nione bandari hii inafanya kazi.” 

Pia, Waziri Mkuu aliwataka raia wa Burundi wanaohitaji kuingia nchini wahakikishe wanafuata taratibu zote za uhamiaji kabla ya kuingia nchini. “Sisi Tanzania na Burundi ni ndugu, ili kudumisha amani na kuimarisha ujirani mwema kila mmoja afuate sheria na taratibu zilizopo.” 

Kadhalika, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kigoma, Pendo Mangali ahakikishe anashughulikia madai ya vijana waliokuwa wanafanyakazi za vibarua katika ujenzi wa miradi hiyo ya maendeleo wanalipwa stahiki zao. 

"Mkurugenzi hapa lazima uje tena, kajipange Jumatatu tarehe 21 Desemba, 2020 uje hapa ukutane na walalamikaji wote uratibu vizuri ili hawa wapate haki zao na Mheshimiwa Mkuu wa wilaya simamia hawa vijana wapate stahili yao,"

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news