Waziri wa Elimu Zanzibar arejea wito wa usafi

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohamed Said amesema, kuna umuhinu mkubwa wa kufaya usafi wa mazingira katika maeneo yanayowazunguka ili kujikinga na maradhi mbalimbali, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Akizungumza wakati wa zoezi maalum la usafi wa mazingira kwa watendaji wote wa Wizara ya Elimu Zanzibar, Waziri Simai amesema uwajibikaji kazini unahitaji mazingira safi na salama.

Amesema, wananchi wa Zanzibar wakiwa na utamaduni wa kuwa na siku maalum ya kufanya usafi katika maeneo mbalimbali kutaisaidia nchi kua na miji safi.

Aidha, amewapongeza watumishi wote wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kuitikia wito na kuhudhuria kwa wingi katika zoezi la usafi ambalo limeleta muonekano mzuri katika wizara yao.

Amewataka kuhakikisha kuwa zoezi hilo linakuwa endelevu ili kuweka mazingira safi na salama.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dkt.Idrisa Muslim Hija amesema ni muda wa wananchi wote wa Zanzibar kuendeleza utamaduni wa usafi kwani usafi ni ibada katika dini zote.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bi. Nabila Habibu amempongeza Waziri wao kwa kuanzisha zoezi hilo na kufanya wizara yao kua mfano kwa wizara nyingine katika kudumisha usafi ofisini.

Wakati huo huo Mhe Simai ameshiriki usafi wa mzingira katika Taasisi ya Sayansi Karume na kuwataka wanafunzi waliopo ndani ya dakhalia wa taasisi hiyo na kwingine kuhakikisha wanafanya usafi kila wiki ili kujiepusha na maradhi mbalimbali yakiwemo ya milipuko.

Kwa upande wao wanafunzi wa Dakhalia ya Taasisi ya Sayansi Karume (KIST) wamekiri kuwepo kwa mazingira machafu ndani ya dakhalia yao ambapo wameahidi kusafisha ili waondokane na muonekano mbaya wa dakhalia zao.

Katika hatua nyingine zoezi kama hilo limefanyika katika ofisini mbalimbali za Wizara ya Elimu Pemba ambapo Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo, Maalim Mohammed Nassor ameliongoza.

Zoezi la usafi wa mazingira limefanyika katika idara na taasisi zote za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na litaendelea kufanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ili kuepusha ofisi kuwa na muonekano mbaya.

Post a Comment

0 Comments