William Barr:Uchaguzi wa Marekani haukuwa na udanganyifu

William Barr, Mwanasheria Mkuu wa Marekani amesema kwamba Wizara ya Sheria haijapata ushahidi wowote wa kufanyika udanganyifu katika hesabu ya kura kwa uchaguzi Mkuu wa Marekani uliofanyika Novemba 3 mwaka huu wa 2020, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Kwa mujibu wa AP, Barr amesema kwamba wizara hiyo haijapata sababu yoyote inayoweza kubadlisa matokeo ya uchaguzi huo ambao ulimpa ushindi Rais mteule Joe Biden na Makamu wake Kamala Harris ambao wameahidi kujenga uchumi imara wa Marekani.
Rais Donald Trump (kulia) akiwa na Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr.

Wawili hao ambao wanatarajiwa kuapishwa mwezi ujao kwa sasa wamebaikisha siku 49 tu za kuingia Ikulu ya White House ambapo watatoka kuwa wateule hadi Rais na Makamu wa Rais.

Barr amesema, waendesha mashtaka wa Marekani wamekuwa wakishirikiana na maafisa wa FBI kufuatilia madai yaliyokuwa yametolewa kuhusu uchaguzi huo, lakini hadi sasa hawana ushahidi wowote.

Licha ya hatua hiyo, bado Rais Donald Trump anaendelea kutoa madai kwamba kulifanyika wizi wa kura, na kukataa kukubali kwamba alishindwa na rais mteule Joe Biden.

Barr ni mmoja wa washirika wa karibu wa Rais Donald Trump na aliagiza wanasheria wa serikali kote nchini kuchunguza madai ya wizi wa kura iwapo ulifanyika.

Post a Comment

0 Comments