Yanga SC yaichapa Dodoma Jiji FC 3-1

Wanajangwani, Yanga SC wameendelea kujikusanyia alama katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya Dodoma Jiji FC leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, anaripoti Mwandishi Diramakini (Arusha).
Leo Yanga SC imefikisha alama 40 baada ya kucheza mechi 16 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa alama nane zaidi ya Simba SC ambao wana mechi mbili mkononi kwa sasa.

Chini ya kocha, Mbwana Makatta, timu ya Dodoma Jiji FC ilitangulia kwa bao la mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Seif Abdallah Karihe dakika ya tatu tu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Metacha Boniphace Mnata kufuatia krosi ya Dickson Ambundo kutoka upande wa kushoto. 

Aidha, nahodha na beki Mghana, Lamine Moro ameisawazishia Yanga SC dakika ya 25 baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na Deus Kaseke na kugeuka haraka kumtungua kipa Aaron Kalambo.

Kipindi cha pili kocha wa Yanga SC, Cedric Kaze alikianza kwa kumuingiza mchezaji mpya, Mrundi mwenzake, Said Ntibanzonkiza ambaye alikwenda kuiongezea kasi safu ya ushambuliaji na kupata mabao mawili zaidi. 

Ntibanzonkiza mwenyewe akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 69 kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20 na ushei kufuatia yeye mwenyewe kuangushwa na kiungo Salmin Hoza nje kidogo ya boksi.

Beki mwingine wa kati, Bakari Nondo Mwamnyeto akaifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 75 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Ntibanzonkiza kutoka upande wa kulia kufutia beki Kibwana Shomari kuangushwa na Ambundo. Matokeo hayo yameifanya Dodoma Jiji FC kunabaki nafasi ya 11 kwa alama zake 19 baada ya kucheza mechi 14. 

Wakati huo huo, Desemba 18, 2020 Azam FC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Kata ya Chamazi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke,Dar es Salaam. 

Sare hiyo iliifanya Azam FC ifikishe alama 29 baada ya kucheza mechi 16, ingawa inabaki nafasi ya tatu nyuma ya mabingwa watetezi, Simba SC wenye alama 32 za mechi 14 na vinara, Yanga SC wenye alama 40 za mechi 16. 

Mara mbili Azam FC walitangulia kwa mabao ya Ayoub Lyanga dakika ya 34 na Mudathir Yahya dakika ya 60 na Ruvu Shooting ilisawazisha kupitia kwa Emmanuel Martin dakika ya 53 na Fully Zulu Maganga dakika ya 70.

Mbali na hiyo, mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Biashara United imeichapa Mbeya City 3-0, mabao ya Chrustian Zigah dakika ya 10 na 25 na Derick Mussa dakika ya 68 Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara. 

Wakati huo huo, Kagera Sugar wameibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Kaitaba, Bukoba. 

Mabao ya Kagera Sugar yamefungwa na Nassor Kapama dakika ya 56, Peter Mwalyanzi dakika ya 73 na Saadat Mohamed dakika ya 80, wakati la Coastal Union limefungwa na Abdul Suleiman dakika ya 45 kwa penalti. 

Mchezo uliotangulia mchana bao la dakika ya 90 la Salum Chubi liliinusuru Mwadui FC kulala nyumbani mbele ya Polisi Tanzania iliyotangulia kwa bao la Daruwesh Saliboko dakika ya 17 Uwanja wa Mwadui Complex uliopo Kishapu mkoani Shinyanga.

No comments

Powered by Blogger.