Yanga SC yaichapa Ihefu FC 3-0, Dodoma Jiji, JKT Tanzania zang'ara

Wanajangwani, Yanga SC wamekamilisha mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara bila kupoteza mechi kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Ihefu FC, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Mtanange huo wa leo Desemba 23, 2020 umepigwa katika dimba la Sokoine jijini Mbeya ambapo kwa sasa Yanga SC inafikisha alama 43.

Yanga SC inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya mechi 17 za mzunguko wa kwanza ambapo wachambuzi wa masuala ya michezo wamemueleza Mwandishi Diramakini kuwa, kocha wa Yanga SC, Cedric Kaze anazisoma alama za nyakati ipasavyo.

Wanajangwani hao wapo mbele kwa alama 11 zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi tatu mkononi kwa sasa.

Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Hussein Athumani wa Katavi aliyesaidiwa na Jesse Erasmo wa Morogoro na Abdallah Rashid wa Pwani, hadi mapumziko Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Ihefu FC. 

Deus David Kaseke dakika ya 12 akimalizia kazi ya kiungo mpya, Mrundi Said Ntibanzokiza ndiye aliyeanza kuwasimamisha mashabiki wa Yanga SC.

Aidha, Ntibanzokiza, mchezaji wa zamani wa NEC ya Uholanzi, Cracovia ya Poland, Akhisar Belediyespor ya Uturuki, Caen ya Ufaransa, FC Kaysar ya Kazakhtan na Vital’O ya kwao, Burundi akamsetia mshambuliaji Mburkinabe, Yacouba Songne kufunga bao la pili dakika ya 49.

Baadae kocha Kaze akampumzisha Mrundi mwenzake huyo aliyesajiliwa dirisha dogo, mwezi huu na kumuingiza kiungo wa zamani wa Teneriffe ya Hispania, Farid Mussa na Yanga ikapata bao la tatu lililofungwa na kiungo mwingine mzawa, Feisal Salum dakika ya 60 akimalizia pasi ya Kaseke. 

Wakati huo huo, mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao pekee la Seif Abdallah Karihe dakika ya tatu limeipa Dodoma Jiji FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. 

Na mabao ya mshambuliaji wa zamani wa Simba SC na Azam FC, Daniel Lyanga dakika ya 52 na 74 wakaipa JKT Tanzania ushindi wa 2-0 dhidi ya KMC Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Post a Comment

0 Comments