Aliyekuwa kocha wa Simba SC Sven Vandenbroeck asaini mkataba ASFAR

Mbelgiji Sven Vandenbroeck ambaye alikuwa kocha wa Wekundu wa Msimbazi, Simba SC amesaini kandarasi ya miaka miwili na ASFAR Rabat ya Morocco, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Aliyekuwa kocha mkuu wa Simba SC, Sven Vandenbroeck akisaini kandarasi ya miaka miwili na ASFAR Rabat. (Picha na ASFAR/Diramakini).

Ikifahamika kama The Association Sportive des Forces Armées Royales (ASFAR) ambayo pia huwa inajulikana kama Royal Army Club ni klabu ya nchini Morocco yenye makao yake makuu mjini Rabat.

Klabu hiyo iliasisiwa mwaka 1958 baada tu ya Morocco kujipatia Uhuru wake na ni kati ya klabu maarufu nchini Morocco.

Kocha Vandenbroeck amejiunga na timu hiyo siku chache baada ya kuondoka Simba SC akitoka kuiwezesha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Jumatano baada ya kuitoa FC Platinum kwa jumla ya mabao 4-1 kupitia mtanange uliopigwa katika dimba la Benjamin Mkapa.

Aidha, katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja ndani ya Wekundu wa Msimbazi, Kocha Vandenbroeck ameiwezesha timu hiyo kushinda mataji matatu.

Miongoni mwa mataji hayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC),

Kocha huyo alijiunga na Wekundu wa Msimbazi mwezi Desemba 15, 2019 akichukua nafasi ya Mbelgiji mwenzake, Patrick Aussems.

Post a Comment

0 Comments