Aweso aagiza vigogo wawili RUWASA wasimamishwe kazi

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga kutengua uteuzi wa Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara, Mhandisi Sadick Chakka na mwenzake wa Wilaya ya Tarime Mhandisi Marwa Murasa kwa kushindwa kusimamia vyema utekelezwaji wa miradi, anaripoti Mohamed Seif (Tarime).
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kulia) akipitia taarifa ya miradi ya maji inayotekelezwa Wilayani Tarime. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Mara, Mhandisi Sadick.

Maelekezo hayo yametolewa wilayani Tarime, Januari 5, 2021 alipokuwa kwenye mradi wa maji wa Magoto ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani Mara baada ya kutoridhishwa na utekelezwaji wa miradi ukiwemo mradi huo. 

Awali akipokea taarifa ya miradi ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Waziri Aweso amesisitiza kwamba taarifa haina uhalisia na aliwaelekeza wataalam hao kueleza hali halisi ya miradi na sio kudanganya. 
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (katikati) akijadiliana jambo na Mbunge wa Tarime Vijijini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri.

Akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa taarifa, Mbunge wa Tarime Vijijini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara ambaye aliambatana na Waziri Aweso amemueleza juu ya adha ya huduma ya maji inayowasumbua wananchi wa Tarime.

Mwita amesema kwamba miradi mingi ya maji wilayani Tarime ina changamoto na hivyo alimuomba Waziri Aweso kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaohusika kuchelewesha utekelezwaji wa miradi.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kulia) akikagua chanzo cha maji mradi wa Magoto. Kushoto ni Mbunge wa Tarime Vijijini na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwita Waitara. 

Taarifa ya miradi sambamba na maelezo ya Naibu Waziri, Mwita na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri kuhusu hali halisi ya miradi ya maji wilayani humo ilimchafua Waziri Aweso na amelazimika kutofuata ratiba ya kukagua miradi iliyokuwa imepangwa na wataalam hao na badala yake alielekeza kupelekwa kwenye miradi mingine yenye changamoto ambayo haipo kwenye ratiba. 

"Nimepitia taarifa ya wataalam wetu hapa na hii ratiba waliyopanga sikubaliani nayo, sasa nataka mnipeleke kwenye miradi mingine na siyo hii mliojipangia nyinyi ili tu kunifurahisha,” Waziri Aweso amewaelekeza wataalam hao.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizungumza na wananchi wanaonufaika na mradi wa Magoto. Kulia ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyakonga, John Magogo.

Waziri Aweso amejadili taarifa hiyo ya utekelezwaji wa miradi wilayani Tarime na huku akimtaka Meneja huyo wa Mkoa kueleza hali ya mradi mmoja baada ya mwingine na huku akibainisha kiasi cha fedha kilichopo kwenye akaunti ambacho kilipaswa kuwa kimetumika kutekeleza miradi.

“Bora hata kisingizio ingekua fedha kama ambavyo hua mnadanganya lakini sasa hapa Mkoani Mara tumeleta zaidi ya shilingi bilioni nane na fedha iliyopo kwenye akaunti kwa sasa ni zaidi ya shilingi bilioni 3 hivi ni nani atakuelewa watu hawana maji wewe kwenye akaunti unayo fedha ya kutosha,”amehoji Waziri Aweso.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akisisitiza jambo wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa Magoto Wilayani Tarime Mkoani Mara.

Amesema, lengo la kuanzisha RUWASA ni kuhakikisha wananchi wanapata maji na kwamba maelekezo ya awali ni kwamba kabla utekelezwaji wa miradi haujaanza kila Meneja wa RUWASA Mkoa alipaswa kuwasilisha taarifa ya kuainisha miradi kichefuchefu yaani miradi iliyokuwa ni kero kwa wananchi, lakini RUWASA Mkoa wa Mara haikufanya hivyo.

“Wananchi wanachohitaji ni maji bombani, hatutokubali kumuona Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli akiumia na kusononeka kuona wananchi wake wanateseka hawana maji na sisi tupo, hii haipendezi hata mbele za Mungu, tumemuahidi kufanya kazi na sasa tunahakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika ya majisafi na salama,” amesema Waziri Aweso. 

Ameongeza kuwa, taarifa ya hali ya miradi wilayani humo inasikitisha kwani tathmini aliyoifanya inaonyesha miradi mingi imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90, lakini haitoi maji na hivyo aliwataka wataalam kote nchini kutumia vyema utaalamu wao badala ya kujiamulia kujenga miradi kiholela.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza kwa njia ya simu na Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa Magoto. Wanaoshuhudia ni wananchi wanaonufaika na mradi huo. 

“Haiwezekani mradi upo asilimia 98 na hautoi maji, unawezaje kujenga tenki wakati hauna uhakika kama maji yapo? Ulipaswa kujiridhisha na chanzo chako kwanza ili kuhakikisha maji yapo ya kutosha na hatua zingine zinafuata,” amesisitiza Waziri Aweso.

Baada ya mahojiano ya muda mrefu na Mameneja hao kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Waziri Aweso alielekeza msafara alioambatana nao kutembelea mradi wa maji wa Magoto ili kujionea hali halisi ya utekelezwaji wake.

Aidha, mara baada ya kutembelea mradi huo na kujionea hali halisi sambamba na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo, Waziri Aweso alijiridhisha bils shaka kwamba mradi huo haujatekelezwa kama inavyopasa.
Wananchi wa Kata ya Nyakonga wakimsikiliza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa maji wa Magoto unaonufaisha vijiji vya Magoto na Nyakonga.

Hali hiyo kwa ujumla na taarifa iliyowasilishwa kwake hapo awali pamoja na maelezo ya viongozi na wananchi wa Kata ya Nyakonga ilipelekea Waziri Aweso kumuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kutengua uteuzi wa Mameneja hao na alimtaka kufika mkoani Mara ili kujionea hali ya miradi sambamba na kuunda kamati itakayochunguza miradi kichefuchefu yote mkoani humo.

“Namuelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Maji kutengua uteuzi wa Mameneja hawa mara moja na wapewe wengine watakaomudu majukumu haya ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika na toshelevu,”ameelekeza Waziri Aweso.

Amesema, miradi mingi mkoani Mara hairidhishi na hivyo ni muhimu Katibu Mkuu akaitupia jicho RUWASA hususan watendaji wake na kwamba wasiokuwa na uwezo waondolewe na alisisitiza kwamba ni muhimu kujiridhisha uwezo wa wataalam kabla ya kuwapanga.

Waziri Aweso vilevile ameelekeza miradi yote ya maji iwe shirikishi, viongozi na wananchi wa maeneo husika wawe na uelewe wa pamoja wa kinachoendelea ili kuepuka kucheleweshwa ujenzi wake.

Waziri Aweso yupo Mkoani Mara kwa ziara ya siku tatu ya kukagua miradi ya maji hususan inayotekelezwa maeneo ya vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news