Chuo cha Reli Tabora chatakiwa kuongeza kozi za reli zinazoendana na mabadiliko

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya, amezungumzia umuhimu wa Chuo cha Reli Tabora kuongeza kozi za reli zinazoendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ili kuzalisha wataalam wengi wa reli wataohudumu katika miradi mikubwa ya reli inayoendelea kujengwa nchini, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa uongozi wa Chuo cha Reli cha Tabora na watalaamu wa karakana ya reli iliyopo mkoani humo. 
Mhandisi Mitambo kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Edgar Bakuza, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua namna ya ukarabati na matengeneo ya vichwa vya treni unaofanyika katika karakana ya reli iliyopo mkoani Tabora. 

Ameyasema hayo mkoani Tabora, wakati alipokagua chuo hicho na karakana ya reli ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza kuwepo kwa mikakati madhubuti ya kulisaidia Taifa katika usimamizi na ujenzi wa miundombinu ya reli mpya ya kisasa na ile ya reli ya kati inayoendelea kuboreshwa. 

“Huu ni wakati wa Shirika la Reli nchini ( TRC), pamoja na Taasisi zake kuja na mtazamo mpya utakaowezesha juhudi za Serikali za kufufua Sekta ya Reli kufanikiwa,”amesema Mhandisi Kasekenya. 
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akimsikiliza na Mhandisi Mitambo kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Edgar Bakuza wakati alipokagua karakana ya reli, mkoani Tabora. 

Aidha ameitaka TRC kuhakikisha inaboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili fedha inayopatikana iwezeshe kuboresha huduma zake na kupata faida. 

Kasekenya ameeleza lengo la Serikali ni kuhakikisha mizigo mizito inasafirishwa kwa reli nchini kote ili kulinda barabara. 
Mkuu wa Chuo cha Reli, Bw. Damas Mwajanga, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua karakana ya reli, mkoani Tabora.

Aidha, Naibu Waziri Kasekenya amesisitiza umuhimu wa watumishi wa reli waliopo kazini kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuondoa kufanya kazi kwa mazoea. 

Amewataka watumishi wa reli kuwa waadilifu na kuacha vitendo vyote vya rushwa na uhujumu ili kuiwezesha reli kuwa salama wakati wote. 
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akishuka katika moja ya kichwa cha treni kinachofanyiwa matengenezo katika karakana ya reli, mkoani Tabora. Naibu Waziri Kasekenya alikagua utendaji kazi wa karakana hiyo. 

“Hakikisheni huduma za reli zinakuwa za haraka na uhakika, punguzeni urasimu kwa wafanyabiashara”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya. 

Naye Mkuu wa Chuo cha Reli Tabora, Bw. Damas Mwajanga, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa chuo hicho tayari kimepata ithibati ya NACTE na hivyo kimeanza kuongeza udahili wa wanafunzi ili kuweza kuhudumia soko la reli katika Ukanda wa Afrika Mashariki. 
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Chuo cha Reli Tanzania, mkoani Tabora. 

Zaidi ya wanafunzi 200 wa ngazi za cheti na diploma wanasomea mafunzo ya reli katika kampasi zake za Tabora na Morogoro. 

Chuo cha Reli cha Tabora kilianzishwa mwaka 1947 ikiwa ni kituo kikuu cha kuhudumia reli katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kimekuwa kikitoa mafunzo ya ufundi wa treni, udereva wa treni, umeme, watalaam wa mawasiliano ya treni na wakaguzi wa mabehewa.

Post a Comment

0 Comments